2015-11-19 15:13:00

Papa Francisko ni Baba wa Maskini na Mtetezi wa wanyonge!


Askofu Paul Kariuki wa Jimbo Katoliki Embu, Kenya anasema, Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya viongozi wa Kanisa ambao wamekuwa mstari wa mbele kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai kwa kuhakikisha kwamba, wagonjwa, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wanapewa huduma makini kama kielelezo cha imani tendaji na ushuhuda wa upendo wao kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa Katoliki nchini Kenya ni mdau mkubwa wa huduma ya afya na kwamba inamiliki walau asilimia 30 ya Hospitali zote zilizoko nchini Kenya.

Hii ni sehemu muhimu sana ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu kama ambavyo Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakazia. Hapa anasema Askofu Kariuki, sayansi na imani vinawekwa pamoja kwa ajili ya huduma kwa binadamu na kwamba, hakuna sababu ya kuwepo na kinzani wala misigano kwani lengo ni ustawi na maendeleo ya binadamu kiroho na kimwili.

Huduma ya afya ikisindikizwa na imani tendaji, hapo kuna uwezekano wa kupata mafanikio makubwa na kwamba, hiki kinaweza kuwa ni kielelezo cha ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika huduma makini, kiasi cha wafanyakazi katika sekta ya afya kutumia ujuzi, maarifa na weledi wao kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa. Askofu Paul Kariuki anakaza kusema, kuna haja kwa waamini kuhakikisha kwamba, huduma yao kwa wagonjwa na vipaumbele vyao vinaongozwa pia na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Waamini kamwe wasiogope wala kukatishwa tama wanaposimama kidete kulinda na kutetea Mafundisho Jamii ya Kanisa katika medani mbali mbali za maisha, kwani lengo ni kukuza na kudumisha kwanza kabisa: utu, heshima, haki, amani na mafao ya wengi. Lakini Mafundisho Jamii ya Kanisa ni muhimu sana kwa wafanyakazi katika sekta ya afya ambako maisha ya mwanadamu yako hatarini daima, bila kusahau pia umuhimu wake katika vyombo vya sheria na mahakama; mahali ambapo haki inapaswa kupewa msukumo wa pekee.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kuanzia tarehe 25 – 30 Novemba 2015, iwe ni fursa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kurejea tena na tena katika nyaraka muhimu sana za Kanisa kuhusu maisha ya binadamu kama ile iliyotolewa na Mwenyeheri Paulo VI: Maisha ya binadamu, “Humane vitae” na ile ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Injili ya uhai, “Evangelium vitae” bila kusahau nyaraka ambazo zinagusa pia maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika kama vile: Kanisa Barani Afrika, Ecclesiae in Africa; Dhamana ya Afrika, “Africae munus” inayojikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho, changamoto pevu sana Barani Afrika.

Familia ya Mungu Barani Afrika inachangamotishwa kusimama kidete kulinda na kutetea kanuni maadili na utu wema kadiri ya mila na desturi njema za Kiafrika na kamwe isitumbukizwe katika mmong’onyoko wa maadili na utu wema kwa kukumbatia mambo ambayo ni kinyume kabisa na tunu bora za maisha Barani Afrika. Utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba na kifo laini; ukanimungu pamoja na ndoa za watu wa jinsia moja ni mambo ambayo ni hatari sana kwa maisha na utume wa Familia ya Mungu Barani Afrika na kamwe hivi si vipaumbele vya Bara la Afrika.

Askofu Paul Kariuki ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anakaza kusema, Kenya kama zilivyo nchini nyingine Barani Afrika inahitaji kupambana kufa na kupona ili kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga kadiri ya malengo ya Umoja wa Mataifa, sanjari na kuongeza bajeti kwenye sekta ya afya kuliko hali ya sasa ambako Serikali imetenga kiasi cha asilimia 7.9% ya bajeti nzima. Kuna haja ya kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi pamoja na kuwasaidia waathirika wa ugonjwa huu kwa hali na mali.

Umefika wakati kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kuwaheshimu na kuwathamini wanawake ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya familia zao: kiroho na kimwili. Wanawake ni madhabahu makuu ya Injili ya uhai, wakiheshimiwa, watakuwa ni wadau wa kwanza katika kulinda na kutetea Injili ya uhai, wasipothaminiwa, watatumiwa na wajanja wachache kuwa ni vichokoo na vyombo vya mauaji ya watoto wasiokuwa na hatia; watoto wanaopaswa kutunzwa na kulelewa tangu wakiwa bado tumboni mwa mama zao!

Madaktari wanaotoa huduma ya tiba na kinga, waongozwe na dhamiri nyofu, tayari kulinda na kutetea maisha ya binadamu na kamwe wasiburuzwe na mambo ambayo yanasigana na utu wema pamoja na dhamiri nyofu! Mazingira ya kazi na huduma katika sekta ya afya yaendelee kuboreshwa zaidi, binadamu na utu wake wakipewa kipaumbele cha kwanza na wala si uchu wa fedha na faida kubwa.Wahudumu katika sekta ya afya watekeleze dhamana na majukumu yao kwa kuzingatia kanuni maadili, sheria na dhamiri nyofu. Serikali pia itekeleze wajibu wake kwa kuwalipa vyema, ili kuondokana na kishawishi cha rushwa na hujuma hospitalini. Wawe ni waaminifu, wakweli na wacha Mungu wanapohudumia Injili ya uhai!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa ZENIT.








All the contents on this site are copyrighted ©.