2015-11-18 14:53:00

Papa : Jubilee ya Huruma ya Mungu i karibu, takasenyi mioyo


Mafundisho ya Papa Francisco kwa Jumatano hii kwa mahujaji na wageni yamelenga zaidi katika uwepo wa Mwaka maalum wa Jubilee ya Huruma ya Mungu, ambao Mama Kanisa anaanza maadhimisho yake hivi karibuni, hapo Desemba 8 , 2015, ambayo ni Sikukuu ya Bikira Maria kuzaliwa bila dhambi ya Asili. 

Katika mtazamo huo,  Papa aliianza Katekesi  kwa kutoa mwaliko kwa wote, akisema,  Katekesi hii imetufikisha mbele ya Mlango , si tu Mlango Mtakatifu , lakini pia Mlango mkubwa , unaotupeleka katika Huruma ya Mungu , Mlango wenye yote mazuri , Mlango wa toba  na wenye  sadaka  ya  neema ya msamaha wa Mungu. Aliendelea kuutaja kuwa ni  Mlango uliofunguliwa wazi kwa ukarimu, na kinachotakiwa kutoka wetu ni kuwa na 'ujasiri wa kuvivuka vizingiti vinavyotuzuia  kupita katika mlango huo.  Vizingiti vya dhambi vinavyokuwa kikwazo katika kuupita Mlango huu wa huruma ya Mungu.

Papa ameleza na kumtaka kila mmoja, apime dhamira yake , kuyaona yaliyomo ndani ya roho, dhambi zenye kuweka giza  katika kuupita Mlango Mtakatifu wa Huruma ya Mungu.  Pia ameonya kwamba , hakuna sababu ya kuona aibu kuomba msamaha kwa Mungu , kwa kuwa sisi sote ni  wenye dhambi! Na hivyo inafaa kunufaika na  wakati huu, kupata ujasiri wa kuvuka vizingiti na kuomba msamaha na huruma ya Mungu , ambaye  kamwe hachoki kusamehe, kamwe hachoki kusubiri! Yeye  anayeonekana kwetu sisi, yeye daima aliye kando yetu.  Kinachohitajika tu ni sisi kuwa na ujasiri wa kulivuka lango  hili!

Papa aliendelea na Katekesi yake kwa kurejea pia Sinodi ya Maaskofu ya mwezi  Oktoba mwaka jana, akisema  jamii yote  na Kanisa zima, ilihimizwa kuutafuta Mlango wa Huruma ya Mungu, ambao daima ni wazi kwa watu wote. Kanisa lilihimizwa kufungua milango yake wazi kwa wote na pia kutoka , kutoka na kwenda   kukutana na  wote na kuwaleta kwa Bwana,  wake wa waume walio katika hija ya maisha , ambao wakati mwingine wamepoteza matumaini na uhakika, hasa katika nyakati hizi ngumu. Papa alikumbusha kwamba,  Familia za Kikristo, zilitiwa sana  moyo kufungua mlango wa Bwana ambaye anasubiri nje tayari kuingia ndani na kuwariwaza na baraka zake na kujenga urafiki nao.  Kama ulivyo mlango wa huruma ya Mungu daima ni wazi, hata milango ya makanisa yetu, upendo wetu kwa jamii zetu, Parokia zetu, taasisi zetu, Majimbo yetu ni lazima yajifunue wazi kwa wote na hivyo basi kuwa tayari kwenda nje, na kuwaleta wengine katika  huruma ya Mungu.  Amesema , Jubilee hii  ina maana kwamba, mlango mkubwa wa huruma ya Mungu ni wazi,na ndivyo inavyoèpaswa hata  pia milango midogo ya makanisa yetu kuwa wazi kuhudumia watu wote kiroho na kihali pia. Kuweka  wazi, ili Bwana aweze kuingia ndani , au kuwatoe nje wale waliofungwa katika gereza la dhambi , gereza la ubinafsi na dhambi nyingine nyingi.

Papa aliendelea kuasa kwamba,  kamwe Bwana halazimishi mtu kupita katika mlango huu Mtakatifu wa Maisha, lakini daima kiroho  hubisha hodi  na kusubiri ruhusa ya kuingia ili ayatawale maisha yetu , utawala wenye kutuletea furaha kamili katika maisha.  Papa alieleza na kuwatahadharisha waamini kwamba, wanapowaendea watu,  kuwapa habari njema za kupita katika mlango huu wa maisha ya furaha isiwe kwa kulazimisha ,lakini kuzungumza nao  kwa unyenyekevu na upole wote, hasa kwa njia ya utendaji ili wasioamini waweze kuona mfano wa maisha hayo ya furaha  wanayo yatangaza na kuyaishi ili wapate kuiamini Injili ya Yesu Kristo. 

Alisisitiza, Yesu ndiye Lango kuu la maisha  ambalo wezi hawawezi kulipita. Sote tunapaswa kuisikiliza sauti ya Yesu inayobisha hodi katika nyonyo zetu, sauti yenye kutuhakikishia kwamba tutakuwa salama zaidi kwa kuishi naye. Tunaweza kuingia bila hofu na kutoka bila hatari. Papa alieleza na kuwageukia viongozi wa Kanisa akisema wana jukumu la kufungua milango yote kama  Mchungaji Mwema (sawa na Yohana 10.2). Wao kama waangalizi  wanapaswa kuisikiliza sauti ya Mchungaji Mkuu , na kuufungua Mlango ili kondoo wote waweze pita na kama kuna mmoja aliyepotea ni lazima kwenda kumtafuta mahali popote alipopotelea.

Katika roho hii, Papa alikamilisha katekesi  yake ,  sisi sote tunakaribia kuianza  Jubilee, yenye kutupeleka katika Mlango Mtakatifu, ambako  kuna mlango mkubwa wa huruma zake Mungu , mlango wa kiroho wenye  kutupatia msamaha wa Mungu, kwa dhambi zetu na wenye kuwakaribisha wote wanaobisha hodi.. .

Baada ya Katekesi hiyo, Papa alitoa ombi lake kwa ajili ya Siku ya  Haki za Mtoto Duniani , inayoadhimishwa siku ya Ijumaa,20 Novemba, akisema ni   wajibu wa kila mtu kuwalinda watoto dhidi ya aina zote za madhulumu na unyanyasaji  unaoweza wanyima haki kukua vyema. Kila mmoja anapaswa kuzingatia haki zote zinazofanikisha mazuri yote kwa watoto,  ili kwamba, kusiwe na mtoto yoyote anayekabiliwa na aina yoyote utumwa au  unyanyasaji. Papa ameonyesha matumaini yake kwamba,  jumuiya ya kimataifa iko macho na hali ya maisha ya watoto, hasa pale ambapo kunapoonyesha dalili za uwepo wa madhulumu ya wazi kwa watoto, kwa  mfano kuajiriwa na makundi ya waasi. Na pia ameikumbusha jumuiya ya kimataifa kwamba, inao wajibu wa kusaidia familia ili kuhakikisha kila mtoto anaandikishwa shule na kupata  elimu bora kama haki yake.

Pia Papa ametoa wito kwa waamini wote kukumbuka tarehe 21 Novemba, ambamo  Mama Kanisa  Kanisa huadhimisha Siku Kuu ya Maria kuwasilishwa hekaluni, kutoa shukurani kwa Bwana,  kwa ajili ya zawadi ya wito wa wanaume na wanawake, walio yatolewa maisha yao sadaka kwa Mungu , wakiishi katika hali ya ukimya kwenye majengo ya  monasteri na nyumba za kitawa, ili waweze kutimiza dhamira ya ya maombi yao na kazi za kimyakimya, na wakati huohuo wakiusikia ukaribu wa waamini kiroho na kimwili pia. .

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.