2015-11-18 14:28:00

Mti wa Noeli utazinduliwa wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu


Mti wa Noeli kwa ajili ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa mwaka 2015 umetolewa kutoka Ujerumani na utawekwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wote wa Kipindi cha Majilio na Noeli. Mti huu ni zawadi kutoka Mkoa wa Trento kwa kushirikiana na Marafiki wa Mapango ya Noeli kutoka Tesero.

Taarifa hii imetolewa na utawala wa mji wa Vatican unaokaza kusema, mti wa Noeli unatarajiwa kuwasili mjini Vatican kati ya usiku wa tarehe 18 Novemba kuamkia tarehe 19 Novemba 2015. Pango la Noeli litatengenezwa na wafanyakazi pamoja na wataalam wa Bustan ya Vatican. Mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wataweza kuuona mti huu kuanzia tarehe 8 Desemba 2015 wakati Mama Kanisa atakapokuwa anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Kukingiwa Dhambi ya Asili, sanjari na uzinduzi wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Taa zitakazotumika kwenye Pango la Noeli kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican zitawashwa rasmi hapo tarehe 18 Desemba 2015. Mti wa Noeli kwa mwaka huu utapambwa zaidi kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na watoto wagonjwa wa Saratani wanaohudumiwa kwenye Hospitali mbali mbali nchini Italia. Ni mti utakaopambwa kwa sala na matashi kutoka kwa watoto na wazazi wao kazi ambayo imeratibiwa na Mfuko wa Lene Thun. Mazingira ya Pango la Noeli kwa mwaka huu yatagusa kwa namna ya pekee maisha ya watu kijijini huko Trento, Kaskazini mwa Italia, kwa kuonesha pia umuhimu wa Jumuiya ya waamini kujikita katika matendo ya huruma, hususan huduma kwa wagonjwa, maskini na wazee.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.