2015-11-17 11:42:00

Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania


Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania anatarajiwa wakati wowote kutangaza jina la Waziri mkuu mteule, tayari kupigiwa kura na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo limeanza kikao chake cha kwanza tarehe 17 Novemba 2015. Kikao hiki kimemchagua Mheshimiwa Job Ndugai kutoka Chama cha Mapinduzi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuwabwaga wagombea wengine kutoka kwenye vyama vya upinzani. Tayari amekula kiapo cha uaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Spika Job Ndugai kutoka Jimbo la uchaguzi la Kongwa, Dodoma, kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015 amekuwa ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Itakumbukwa kwamba, kadiri ya Katiba wabunge wote kwa jumla ni 394, lakini majimbo yaliyofanikisha uchaguzi mkuu hapo tarehe 25 Oktoba 2015 yalikuwa ni majimbo 257, kumbe, bado kuna majimbo 7 yanayopaswa kufanya uchaguzi mdogo. Bunge la 11 lina changamoto nyingi zinazoendelea kuikabili Tanzania kwa wakati huu: Mosi ni kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa; uwepo wa idadi kubwa ya wabunge kutoka vyama vya upinzani; wasomi vijana; lakini yote haya yanapaswa kusaidia mchakato wa kuwapatia watanzania maendeleo endelevu! Spika wa Bunge Job Ndugai anasema, kauli inayoongoza kazi yake ni “Sasa kazi tu”. Rais Magufuli anatarajiwa kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapo tarehe 19 Novemba 2015 na hapo atatoa dira na vipaumbele katika Serikali yake, hotuba inayosubiriwa na watanzania wengi ndani na nje ya Tanzania.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amepokea salamu za pongezi kutoka kwa Malkia Elizabeth II wa Uingereza kufuatia kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika salamu hizo Malkia wa Uingereza amemueleza Mhe. Rais Dkt. Magufuli kuwa “Natumaini kuwa mahusiano baina ya nchi hizi mbili ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Madola yataendelea wakati wa utawala wako, nakutakia kheri pamoja na wananchi wa Tanzania” amesema malkia katika salamu zake.

Salamu pia zimetoka kwa Mfalme Akihito wa Japan ambaye amemueleza Mhe. Rais Dkt. Magufuli “Nakutumia salamu za dhati, mafanikio na furaha kwako Mheshimiwa Rais na watu wa nchi yako” Amesema. Salamu zingine kwa Mhe. Rais Dkt. Magufuli zimetoka kwa Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kiarabu ya Saharawi, Mhe. Mohamed Abdelaziz ambaye amemtakia kheri Mhe. Rais Dkt. Magufuli na kumueleza kuwa “Nina imani kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea vyema chini ya uongozi wako kuelekea katika kupata maendeleo na mafanikio zaidi”. Amesema; na pia amekipongeza Chama Cha Mapinduzi na Watanzania kwa uchaguzi wa kidemokrasia ulioendeshwa katika mazingira ya kistaarabu chini ya usimamizi wa waangalizi kutoka kwenye kanda, bara na kimataifa na hivyo kuliletea sifa bara la Afrika.

Mhe. Rais Dkt. Magufuli pia amepokea salamu kutoka kwa Rais wa Namibia Mhe. Hage Geingob na kumueleza Mhe. Rais Dkt. Magufuli kuwa salamu zake na zile za wananchi wa Namibia ni za dhati kwa Serikali na Watanzania kwa ujumla kwa ushindi wa kiti cha Urais. “Pia napenda kutoa pongezi kwa Chama Cha Mapinduzi kwa ushindi uliopatikana katika uchaguzi wa Oktoba 25, 2015”.Amesema na kuongeza kuwa “Kwa hakika Watanzania wamezungumza na kukipa tena CCM Mamlaka ya kuipeleka mbele Tanzania kuelekea kwenye mafanikio zaidi”. Ameongeza.

Salamu zingine ni kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye amesema Tanzania kwa mara nyingine tena imedhihirisha kuwa ni nguzo ya demokrasia barani Afrika. Naye Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Joachim Gauck amemtakia Mhe. Rais Dkt. Magufuli na Watanzania kwa ujumla mafanikio katika kuendeleza Taifa kwa ujumla.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.