2015-11-17 09:39:00

Afrika ya Kusini yakumbwa na ukame wa kutisha!


Serikali ya Afrika ya Kusini inasema kwamba, kuna ukame wa kutisha unaoikabili Afrika ya Kusini kwa sasa, kiasi cha kusababisha upungufu mkubwa wa maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu, mifugo na shughuli za kilimo cha umwagiliaji. Ukame huu ni matokeo ya kupanda kwa kiasi kikubwa cha joto ambacho hakijawahi kutokea Afrika ya Kusini tangu mwaka 1982. Maeneo ambayo kwa sasa yameathirika kwa kiasi kikubwa nchini Afrika ya Kusini ni yale yaliyoko: Kaskazini Magharibi; Kwazulu-Natal, Mpumalanga, Limpopo na Free State. Serikali ya Afrika ya Kusini inakaza kusema, hili ni eneo ambalo linakaliwa na wananchi zaidi ya 6, 500 na ambalo linajihusisha kwa kiasi kikubwa na shughuli za kilimo cha mahindi.

Ili kukabiliana na changamoto katika sekta ya kilimo, Serikali imetoa ruzuku ya Euro 130, 000. Uzalishaji wa mahindi umeshuka sana anasema Senzeni Zokwana, Waziri wa kilimo, lakini bado kuna akiba kubwa ya mahindi inayoweza kutumika hadi ifikapo mwezi Aprili, 2016. Wizara ya ushirikiano imewahakikishia wananchi wa Afrika ya Kusini upatikanaji wa nishati ya umeme licha ya kupungua kwa maji kwenye mabwawa yanyozalisha nishati ya umeme Afrika ya Kusini. Kiwango cha maji kwenye mabwawa kimeshuka hadi kufikia asilimia 66%.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.