2015-11-16 14:36:00

Watawa ni majembe ya nguvu katika maisha na utume wa Kanisa!


Mpendwa msikilizaji kipindi cha Hazina yetu! Amani kwako!! Karibu tuendelee kukitegea sikio kipindi hiki ambapo kwa sasa tunajaribu kupitia mada mbalimbali zinazohusu maisha ya kitawa. Tutakumbuka kwamba, kwa wakati huu tupo katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa, ambapo Baba Mtakatifu amewaalika watawa wote kutafakari historia za mashirika yao kwa moyo wa shukurani, kuishi sasa kwa ukamilifu wote na kuukumbatia wakati ujao kwa matumaini makubwa. Na sisi waamini wote tumehimizwa sana kuyaenzi maisha ya Kitawa ndani ya Kanisa; huku tukijibidisha kuwaombea, kuwapa shime na mazingira mwanana ili watutumikie vizuri.

Leo mpendwa msikilizaji, tunapenda kuingia katika undani kidogo wa maisha ya kitawa. Tutambue kwamba utawa ni wito mtakatifu. Kila mtu anaweza kutamani kuishi maisha ya kitawa, lakini si kila mtu anaweza kuyaishi maisha hayo ya kitawa. Ni Mungu mwenyewe kwa uradhi wake, huwaita watu, huweka mbegu hiyo ya wito wa maisha ya kitawa mioyoni mwao, nao wakiisha kusikia mguso huo na kwa msaada wa neema za Mungu, huitikia sauti ya wito. Hujiunga na maisha ya kitawa katika mashirika mbalimbali kadiri roho anavyowatuma. Katika mashirika hayo, huyo aliyeitwa, huundwa katika safari ndefu sana ya malezi; safari inayomsaidia aliyeitwa kujiratibisha hivi ili aifahamu vema roho ya shirika aliloliingia, na auambate wongofu wa mwenendo ili aweze kurandanda na mfumo wa maisha katika shirika husika  kadiri ya taratibu za Kanisa na miongozo ya shirika.

Katika Kanisa kuna mashirika mbalimbali ya kitawa. Mashirika hayo yanatofautiana kutokana na karama na lengo la Waanzilishi. Yapo mashirika yanayojulikana kwa majina ya Waanzilishi wao, kama vile Wa-Agustiniani, Wa-Benediktini, Wa-Fransiskani au Wa-Dominikani. Na yapo Mashirika pia yanayotambulika tunu  inayoumba roho ya shirika kama vile Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Wamissionari wa Mateso nk. Yapo pia mashirika yanayofuata roho ya Mtakatifu fulani (hata kama mtakatifu huyo hakuanzisha Shirika), yapo pia mashirika yanayojenga uwepo wake katika Sifa au utume wa Bikira Maria. Yapo mashirika yanayojishikamanisha na kazi maalumu, kama vile kufundisha, kuhudumia wagonjwa, kutunza wazee au kuwahudumia maskini. Yapo pia mashirika ya kitawa ambayo yamejitoa kwa ajili ya utume wa sala tu, tena ndani katika utengo na ukimya wa daima.

Kinachoyaunganisha mashirika yote hayo ni kwamba: yote yana msingi wake katika Kristo Yesu na Injili yake. Mashirika yote ya kitawa ndani ya Kanisa, kila mmoja kwa namna yake, yanafafanua, yanaeleza, yanatekeleza, yanamwilisha na yanaishi kipengele walau kimoja wapo cha maisha na utume wa Yesu mwenyewe. Na kwa mantiki hiyo tunaweza kusema kuwa, mashirika yote ya Kitawa ndani ya Kanisa, katika ujumla wake yanashiriki Utume wa Kanisa zima yaani kuleta ukombozi kwa mwanadamu kiroho na kimwili. Huduma ya kila shirika la kitawa hugusa maisha ya mtu mzima.

Sasa, watu walioitwa na Mungu, hujiunga na maisha hayo ya kitawa, lengo lao la  kwanza kabisa la kumfuasa Kristo kwa karibu zaidi ili kuweza kukua zaidi katika ukamilifu, na mwisho kuupata uzima wa milele. Na katika safari hiyo ya ukamilifu, kwa msaada wa neema ya Mungu inayoisindikiza ile roho ya kitawa, na kwa msaada wa wanajumuia wengine,  kwa mtindo mzima wa maisha, na kule kujimwaga katika utumishi mnyoofu na mnyenyekevu;  mtawa anapiga mbio  kuelekea ukamilifu kwa ajili yake binafsi na kwa ajili ya wengine pia. Ndiyo maana, watawa kila siku, usiku na mchana husali kwa ajili ya Kanisa zima.

Pamoja na lengo hilo la kujipatia ukamilifu, kila mtawa kwa kuchochewa na karama maalumu ya shirika na vifungo vya nadhiri zake au ahadi zake kwa Mungu, hujibidisha kuiishi Injili katika namna mbalimbali zinazogusika. Ndio maana katika hao watawa, wapo ambao wanamfuasa Kristo kama Mwalimu, wapo wanaomfuasa Kristo kama tabibu, wapo wanaomfuasa Kristo kama mfariji wa wagonjwa na wenye huzuni, wapo wanaomfuasa Kristo anayetangaza habari njema ya ufalme wa Mungu kama vile wahubiri na wamisionari, wapo wanaomfuasa Kristo anayeshiriki maisha yake pamoja na watu, wapo wanaomfuasa Kristo anayesali na kutafakari.

Hivyo mpendwa msikilizaji, wote ambao tunawaona katika Kanisa kama watawa, lazima watakuwa wanagusa kipengele kimojawapo au baadhi ya hivyo tulivyovitaja. Kwa mantiki hiyo Mashirika ya Kitawa ni vidole vya Kristo mwenyewe. Watawa wanaendeleza huduma za Kristo yuleyule ndani ya Kanisa. Lakini wanafanya hivyo kwa uongozi wa Mungu kwa ruhusa na  uangalizi mkubwa wa mamlaka halali ya Kanisa.

Na tangu zamani hata nyakati zetu hizi, mashirika ya Kitawa yamefanya kazi kubwa sana ndani ya Kanisa. Yametangaza ujumbe wa Kristo kwa namna mbalimbali. Kanisa linajivunia uwepo wa watawa na ndiyo maana mwaka huu limeutenga rasmi kwa ajili ya Watawa. Swali linalobaki ni hili: maisha haya ya Kitawa yalianzaje anzaje katika Kanisa? Kujibu swali hilo, tusikilizane kipindi kijacho. Kukuletea makala hii kutoka Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.