2015-11-16 08:31:00

Waganda wamejipanga vyema kumkaribisha Papa Francisko!


Wananchi wa Uganda katika ujumla wao wanakabiliwa na matatizo na changamoto ambazo wanapaswa kuzifanyia kazi kwa pamoja kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Umaskini, magonjwa na kwa namna ya pekee ugonjwa wa Ukimwi, Malaria na Kifua kikuu; Ujinga, athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa fursa za ajira. Ikiwa kama wananchi wote wa Uganda wataungana pamoja bila kujali tofauti zao za kiimani, kidini, kikabila au mahali anapotoka mtu, wanaweza kugeuza Uganda ikawa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Uganda kuanzia tarehe 27 Novemba kwa muda wa siku mbili ni nafasi kwa Wakristo na Waislam kushikamana kwa pamoja ili kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu miongoni mwa wananchi wa Uganda. “Nanyi mtakuwa mashahidi wangu” ndiyo kauli mbiu ya hija ya Baba Mtakatifu nchini Uganda. Hii ni nafasi muhimu sana katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene sanjari na ujenzi wa madaraja ya watu kukutana, tayari kushirikiana katika kuendeleza mchakato wa kulinda, kutetea na kudumisha haki, amani na upatanisho kati ya wananchi wa Uganda ambao bado wanasumbuliwa na makovu ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo bado inaendelea kufuka moshi!

Baraza kuu la Waislam nchini Uganda katika tamko lake hivi karibuni, linabainisha kwamba, litaungana na Wakristo kumpokea Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya siku mbili nchini Uganda na kwamba, watapata pia nafasi ya kuzungumza naye kwa ajili ya kudumisha haki, amani, utu na heshima ya binadamu. Leo hii waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kushikamana kwa pamoja kwani wanategemeana na kukamilishana katika medani mbali mbali za maisha.

Hakuna mwamini anayeweza kukaa peke peke kama kisiwa, kwani binadamu kwa asili ameumbwa ili kushirikiana na wengine ili kujenga na kudumisha amani, dhidi ya misiamo mikali ya kidini ambayo kwa nyakati hizi imekuwa ni chanzo cha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Waislam na Wakristo nchini Uganda wanaendelea kushirikiana kwa karibu sana katika huduma kwa wananchi wa Uganda. Askofu mkuu Michael Blume, Balozi wa Vatican nchini Uganda alipowasili nchini humo ili kuanza utume wake, aliwatembelea viongozi wakuu wa Baraza la Waislam nchini Uganda na kuwapatia salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Askofu muu Blume alioneshwa pia zawadi ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II alimpatia Alhaji Sajjabi alipomtembelea nchini Uganda kunako mwaka 1993, zawadi ambayo inaendelea kutunzwa kwa heshima zote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CISA.








All the contents on this site are copyrighted ©.