2015-11-14 10:49:00

Neno la Mungu ni chemchemi ya faraja, imani na matumaini!


Kitabu cha Danieli katika Agno la Kale ni mojawapo ya vitabu vinavyoongea kuhusu ufufuko wa wafu. Ni vitabu vinavyowaongoza watu wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele. Baadaye iko wazi kuwa Yesu ndiye anayeondoa dhambi. Wakati wa mavuno ni uhakika wa kuvuna ikiwa talipanda pamoja naye. Tumaini ni fadhila kuu ya Kibiblia. Ni kutumaini kwa matarajio ujio wa ufalme wa Mungu, ufalme wa haki na amani kati ya watu wake. Yule anatetumainia atapata amani na haki hiyo. Kwanini tumaini ni fadhila yenye nguvu kiasi hicho? Tumaini ni tarajio la furaha na katika Biblia ni tarajio la ujenzi wa ufalme waMungu, katika amani na haki. Anayetumaini anatarajia nafasi katika huo ufalme. Ni nini msingi wa tumaini hilo? Ni imani thabiti kwa mkono wa nguvu wa Mungu.

Historia ya wokovu wetu inadhihirisha hilo. Mkono wa Mungu, wenye nguvu, wenye dhihirisho la upendo. Matokeo yake ni furaha. Kwa sababu Mungu ameonesha tayari kwa watu wake. Mkono wa Mungu tayari umefanya kazi kwa watu wake. Angalia historia ya ukombozi wetu, kwa upendo kabisa ametukomboa. Kwa nini tusifurahi? Hivyo katika Biblia tunaona mitazamo miwili iliyo wazi; tunatazama nyuma kiimani na huku tukiwa na matumaini kwa siku zijazo. Waisraeli waliweza kusherehekea jambo hili tangu walipokombolewa; manabii wakawakumbusha juu ya imani na matumaini yajayo. Hali kadhalika sisi Wakristo tunasherehekea Fumbo la Pasaka la Kristo ambapo Mungu ametukomboa na ametuita kwenye maisha ya utakatifu. Kwa sababu hiyo basi tuna uhakika wa kuokoka toka hasira ya Mungu kama tukibaki waaminifu. Hayo aliyofanya Mungu kwa upendo yatuhakikishia matumaini yetu katika skiku zijazo. Ndiyo maana tupo hapa tunasherehekea upendo wa Mungu kwetu kwa matumaini.

Tuangalie tena masomo yetu ya leo. Somo la kwanza na la pili yazungumzia matokeo ya mambo yajayo na tumaini hilo lijalo. Tutaokoka ikiwa tutaishi ile imani, ule upendo aliotushirikisha Mungu. Kitabu cha Danieli kiliandikwa wakati wa utawala wa Assyria (Ashuru) na mfalme mpagani alilazimisha ibada za miungu wake katika Israeli. Watu walikata tamaa. Walipoteza matumaini. Tukumbuke kuwa wakati huu Hekalu lilishabolmolewa na hivi kadiri ya imani ya Waisraeli walipoteza matumaini. Lakini Danieli anakumbusha utukufu wa Mungu uliokuwa ka& yao. Na hii ndiyo dhamira kuu ya leo – (sadaka mpya) wataishi milele na watang’aa kama nyota. Hivyo wanakumbushwa historia yao na kuweka matumaini yao kwa maisha yajayo.

Katika Injili, Yesu anazungumzia mwana wa mtu ajaye ambaye ataweka ufalme wa Mungu. Ndicho tunachokumbushwa leo na kanisa. Fundisho hili ni zaidi ya kukumbuka. Latuita kuliishi kama fumbo ili jambo hilo lionekane kwa watu. Yesu tayari alishakuja ulimwenguni kwa msamaha wa dhambi. Atakapokuja mara ya pili atatukuta katika hali gani? Tuishi kama watu wanaoamini katika Yesu aliyetufundisha na kushuhudia uwepo wa ufalme wa Mungu kati yetu na siyo watu wanaoigiza au wanaokariri tu alichotufundisha Yesu.

Tukumbuke kuwa katika dini yoyote ile tendo la sadaka huonekana kutambulisha imani hiyo kuliko kitu kingine cho chote kile. Kama Wakristo leo, tuna sadaka gani? Hakika sadaka ya Kristo yatangulia. Lakini tunaiishi namna gani? Katika 1 Kor. 3:16 tunasoma kuwa je hamjui yakuwa ninyi ni hekalu la Mungu, na Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Na katika 2Kor. 6:16 tunasoma kuwa tena hekalu la Mungu linapatanaaje na sanamu za miungu wa uongo? Maana sisi ni hekalu la Mungu aliye hai. Ndivyo alivyosema Mungu, nataka kukaa miongoni mwao, na kati yao nitatembea,nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa ni taifa langu.

Padre J. Healey, M.M katika kitabu chake “Hadithi za Kiafrika” anaelezea tendo la upendo lilofanywa na wasichana wa Shule ya Sekondari Muramba katika mkoa wa Gisenyi, Rwanda kama tendo la upendo na matumaini. Namna mpya ya kuishi sadaka ya maisha yetu. Hii ndiyo sadaka mpya na hekalu jipya. Ilitokea kuwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Wahutu na Watutsi, kikundi cha wanaume wenye silaha, kilivunja na kuingia katika shule yao na kuwalazimisha wajipange kadiri ya makabila yao. Wao walikuwa ni jumuiya moja na walipendana sana. Na waliitambua nia mbaya ya wauaji wale. Wauaji walikuwa na nia ya kuwaangamiza kikabila. Hawakutii amri ile. Bila huruma wale wauaji wakawafyatulia risasi na kuua watu 17 na kujeruhi watu wengine 14. Kati yao alifariki pia Sr. Margarita Bosmans, aliyekuwa mkurugenzi wa shule ya jirani aliyejaribu kuwazuia wauaji. Mwandishi wa Waraka kwa Tito 2:11-13 anaandika, maana neema ya Mungu imetokea kwa kuwaokoa watu wote. Nayo inatuongoza kuzuia yasiyo ya Mungu, na kupinga tamaa za kidunia, tupate kuishi duniani hapa kwa kiasi, kwa haki na kwa uchaji wa Mungu, tukingoja heri tunayoitazamia na ufunuo wa utukufu wa Mungu mkuu na wa Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Tumsifu Yesu Kristo,

Pd. R. Mrosso, C.PP.S.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.