2015-11-14 06:43:00

Mshikamano wa upendo na familia nchini Syria!


Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya familia kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 15 Novemba 2015 anatembelea nchini Syria ili kukutana na kuzungumza na familia za Kikristo katika eneo hili ambalo limegeuka kuwa ni uwanja wa vita. Akiwa mjini Damasco, atawapatia waamini Injili ya Luka ambayo imetafsiriwa katika lugha ya Kiarabu, zawadi ambayo Baba Mtakatifu Francisko amezipatia familia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa, iliyoadhimishwa Jimbo kuu la Philadelphia, nchini Marekani, mwezi Septemba 2015.

Katika mkutano huo, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema walichanga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuzisaidia familia zinazoteseka kutokana na vita nchini Syria. Fedha hizi pia zitawasilishwa kwa wahusika wakati wa hija ya kichungaji ya Askofu mkuu Paglia huko Syria. Lengo ni kuonesha mshikamano wa umoja na upendo wakati huu wa kipindi cha baridi ya kimwili, lakini zaidi baridi na mchoko wa kisiasa na kibinadamu unaotishia maisha na usalama wa wengi.

Akiwa nchini Syria, Askofu mkuu Paglia atapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Makanisa, familia na makundi ya waamini wanaoendelea kuteseka kutokana na vita, nyanyaso na dhuluma mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.