2015-11-13 15:28:00

Umoja na mshikamano katika kukabiliana na changamoto za wakimbizi


Mkutano wa siku mbili kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika uliokuwa unajadili kuhusu changamoto kubwa ya wakimbizi Barani Ulaya umehitimishwa kwa changamoto kwa viongozi wa Ulaya kuwa na mwelekeo mpya sanjari na kuharakisha mgawanyo wa wakimbizi na wahamiaji Barani Ulaya na kwamba, viongozi wa Umoja wa Ulaya wanapaswa kuonesha umahiri katika uongozi. Viongozi hawa kwa pamoja wameanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya wakimbizi kutoka Afrika ambao wanaendelea kufurika Barani Ulaya kila kukicha! Kiasi cha Euro billioni 1.8 kimetengwa na kwamba, Norway na Uswiss tayari zimechangia kiasi cha Euro millioni 78. 2. Katika maadhimisho ya mkutano huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Malta liliwaandikia ujumbe viongozi wakuu wa Jumuiya ya Ulaya kwa kuwakumbusha kwamba, binadamu wote wana asili moja na kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Maaskofu wamewapongeza viongozi wa Ulaya kwa kuonesha utashi wa kisiasa wa kutaka kukabiliana na wimbi la wakimbizi na wahamiaji, ili kuweza kupata suluhu ya kudumu. Malta kwa kipindi cha siku mbili imekuwa ni daraja la kuwaunganisha viongozi wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika, ili kujenga na kuimarisha ari na moyo wa ushirikiano na mshikamano kati ya watu; kwa kuheshimiana, huku sheria, kanuni na taratibu za nchi zikipewa msukumo wa pekee.

Maaskofu wanakaza kusema, wakimbizi na wahamiaji ni watu ambao maisha yao hìyako hatarini kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, umaskini, vita na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kutendewa kwa haki na kwamba, wote hawa wanaasili moja kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, viongozi wa Jumuiya ya Ulaya wataendelea kuonesha moyo wa ukarimu kwa kutekeleza ahadi walizotoa wakati wa mkutano na viongozi wa Umoja wa Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.