2015-11-13 15:02:00

Mwenyeheri Padre Francisco de Paula Victor mtu wa watu kwa ajili ya watu!


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, tarehe 14 Novemba 2015 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anamtangaza Padre Francisco de Paula Victor kuwa Mwenyeheri katika Ibada ya Misa Takatifu inayofanyika Jimbo Katoliki la Campanha, nchini Brazil. Huyu ni Padre wa Jimbo aliyeishi kati ya mwaka 1827 na kufariki dunia kunako mwaka 1905. Kwa muda wa miaka hamsini na tatu alihudumia kama Paroko, akawaonesha watu upendo wa Kristo. Kunako tarehe 10 Mei 2012 atakatangazwa kuwa Mtumishi wa Mungu.

Tarehe 5 Juni 2015 Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya Mama Kanisa akatambua nguvu ya Mungu iliyokuwa ikitenda miujiza kwa njia ya Mtumishi wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema Mwenyeheri Francisko de Paula Victor alikuwa Paroko mchapakazi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wanaparokia wake kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu. Alitenda na kuwajibika kama Mchungaji mwema, kadiri ya Moyo wa Yesu Kristo. Alikuwa kweli Padre mnyenyekevu na mpole, alijitaabisha kuwatangazia watu wake Injili ya Kristo si tu kwa maneno, bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha, akaonesha ile karama ya mchungaji mwema na mlezi bora wa vijana.

Katika kipindi cha miaka michache tu, Jimbo Katoliki la Campanha linabahatika tena kushuhudia mwamini mwenzao akitangazwa kuwa Mwenyeheri, kama ilivyotokea kunako tarehe 14 Mei 2013, Kardinali Angelo Amato alipomtangaza Mwenyeheri Francisca de Paula kuwa Mwenyeheri huko Baependi. Hiki ni kielelezo na ushuhuda kwamba, eneo hili lina mashuhuda wengi wa Injili inayojikita katika upendo na huruma ya Mungu.

Mwenyeheri Francisco de Paula Victor, akiwa mdogo alipewa fursa ya kujiendeleza katika ushonaji badala ya kubaki nyumbani na kushughulikia kilimo, lakini huu kwa hakika haukuwa wito wake. Akapambana na vikwazo na majaribuni mengi, akiwa na umri wa miaka ishirini na miwili, akabahatika kuingia Seminarini, akaonesha ukomavu, ukweli na utakatifu wa maisha.

Mwenyeheri Francisko de Paula Victor akiwa na umri wa miaka ishirini na minne, akapewa Daraja Takatifu la Upadre, akavuka kishawishi cha mawazo mgando yaliyokuwa yanajikita katika tabia ya ubaguzi wa rangi. Utakatifu wa Padre Victor unajikita zaidi katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa moyo wa Ibadan a uchaji, alihakikisha kwamba, anaandaa vyema mahubiri yake, kwani hiki kilikuwa ni chakula cha maisha ya kiroho kwa waamini wake.

Padre Victor alikuwa makini kwa kutoa katekesi, ili kuwafunda waamini kuyafahamu Mafumbo ya Kanisa, tayari kuyamwilisha katika hija ya maisha yao hapa duniani. Alikuwa na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria. Alijitahidi kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa makundi makubwa ya watoto, akawa na utume wa pekee kwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kukua katika kanuni maadili na utu wema. Kwa kuguswa na mahitaji ya elimu kwa vijana, akaanzisha shule kwa vijana ambao walitoka katika familia maskini, ili nao waweze kupata elimu ambayo ingeweza kuwakomboa kutoka katika unyonge wao.

Waamini wakatambua utakatifu wa maisha kiasi kwamba baada ya kifo chake miaka ishirini baadaye wakaandika kwa moyo mkuu mbele ya kaburi lake “Maisha yake yalikuwa ni Injili”. Kardinali Amato anakaza kusema, mambo muhimu sana katika maisha ya utakatifu wake yanajikita katika unyenyekevu na kiasi, hakupenda makuu, daima alikuwa kati ya watu kwa ajili ya kuwahudumia kwa upendo na unyenyekevu mkuu.

Padre Francisco de Paula Victor alipofariki dunia, watu wengi waliguswa na kuhudhuria mazishi yake. Aliaga dunia katika hali ya umaskini, lakini akaonesha ushuhuda mkubwa wa Injili iliyomwilishwa katika uhalisia wa maisha yake kwa njia ya huduma. Vitu vyake vichache vikaanza kutunzwa kwa heshima kama masalia matakatifu, kutokana na mfano bora wa maisha ya kipadre na huduma kwa familia ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.