2015-11-12 14:35:00

Wasaidieni maskini katika shida na mahangaiko yao!


Kujiaminisha, kuangalia na kuharakisha ni mambo msingi kwa Familia ya Mtakatifu Luigi Guanella katika hija ya maisha na utume wao hapa duniani, daima wakijitahidi kuonesha ibada kwa Bikira Maria wa msaada wa Mungu. Tayari Kanisa limekwisha adhimisha Jubilei ya miaka mia moja tangu Mtakatifu Guanella alipofariki dunia, tukio ambalo limewaimarisha katika imani, matumaini na mapendo.

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na mahujaji wa familia ya Mtakatifu Guanella, Alhamisi, tarehe 12 Novemba 2015 mjini Vatican. Mtakatifu Guanella alijiaminisha kwa huruma na neema ya Mungu, akaguswa na upendo wa Mungu kiasi cha kumwezesha kuwa na ujasiri wa kukabiliana na vikwazo vya kibinadamu, ili kumwilisha Injili katika maisha. Alionja neema ya Mungu katika maisha yake na akapata tunza makini, jambo la msingi ni kwa waamini kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu katika safari ya maisha yao!

Waamini watambue kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo na yuko karibu na watu wake katika shida na mahangaiko yao ya maisha, mwaliko kwa waamini kukimbilia katika huruma na upendo wake pamoja na kuendelea kutunza ile neema ya Ubatizo waliyojipatia siku ile walipojivika utu mpya na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Kwa njia hii waamini wanaweza kushinda woga na tabia ya kulalalama bila sababu kwani Mungu anawapenda.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujiangalia ndani mwao katika ukweli na upendo tayari kuwapokea wengine kama ndugu na faraja katika maisha. Dunia imesheheni umaskini, ukosefu wa haki msingi za binadamu na upendo. Hapa kuna hja ya kuwa na watu wenye jicho la upendo na matumaini; watu ambao wako tayari kuwafariji wengine katika shida na mahangaiko yao kama alivyofanya Mtakatifu Luigi Guanella.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuharakisha katika kuwahudumia maskini kwani hawa wana upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani umaskini kamwe hauna subira! Kumbe, kuna haja ya kuharakisha katika kuwahudumia maskini kama alivyofanya Bikira Maria alipoharakisha kwenda kwa binamu yake Elizabeth. Waamini wawe wasikivu makini kwa Roho Mtakatifu, ili kuwaendelea maskini, tayari kuwasaidia. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuishukuru Familia ya Mtakatifu Luigi Guanella kwa huduma wanayoifanya kwa maskini na wahitaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.