2015-11-12 10:28:00

Vijana waelimishwe zaidi kuhusu utunzaji bora wa mazingira!


Malezi makini kwa ekolojia, kanuni maadili katika majadiliano na maendeleo endelevu ni kati ya mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na Monsinyo Francesco Follo, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, katika mkutano wa maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa UNESCO. Vatican inatambua na kupongeza mchango wa UNESCO katika mchakato wa kujenga na kudumisha msingi wa amani kwa njia ya elimu, utamaduni na sayansi; mambo msingi katika ustawi na maendeleo ya binadamu wanaoishi duniani, nyumba ya wote!

Kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mjini Paris, Ufaransa kuanzia tarehe 30 Novemba hadi tarehe 11 Desemba 2015, Monsinyo Follo anakaza kusema, UNESCO hadi sasa imechangia kwa kiasi kikubwa kuhamasisha umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote katika medani mbali mbali za kimataifa. Ajenda za Umoja wa Mataifa zinapania pamoja na mambo mengine, kuwasaidia watu kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuwawezesha vijana kutambua madhara yake ili kweli elimu isaidia kuleta mabadiliko makubwa yanayotazamiwa na wengi.

Ikumbukwe kwamba, dunia ni nyumba ya wote na kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, inayopaswa kutumiwa kikamilifu na kwa njia ya uwajibikaji mkubwa, kwani binadamu kwa kiasi kikubwa amechangia sana uharibifu wa mazingira, nyumba ya wote na madhara yake yanajionesha kwa sasa. Vijana waelimishwe utunzaji bora wa mazingira ili waweze kuwajibika kikamilifu kwa sasa na kwa ajili ya siku zijazo. Jamii inapaswa kuwaachia vijana wa kizazi kijacho mazingira bora zaidi kwa ajili ya maisha ya binadamu.Kikao cha thelathini na nane cha UNESCO kimefunguliwa hapo tarehe 3 Novemba na kitakalimishwa hapo tarehe 18 Novemba 2015. 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.