2015-11-12 08:07:00

Jubilei ya miaka 50 ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa India


Kardinali Oswald Gracias, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mumbai katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini India kuanzia tarehe 12 hadi 15 Novemba 2015 kwa kuishirikisha Familia ya Mungu nchini India anasema, hii ni fursa ya kuweza kutafakari na kuzama zaidi juu ya uelewa wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; tayari kuambata mafundisho ya Kanisa na kuwashirikisha wengine upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo kwa njia ya Ekaristi Takatifu.

Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Kwa kushibishwa na upendo wa Kristo, waweze kuwashibisha wengine . Waamini wanataka kukutana na Yesu katika Fumbo la Ekaristi, ili aweze kutoka kimasomaso kuwalisha na kuwashibisha wengine wanaoteseka kutokana na njaa ya mwili inayonyanyasa utu na heshima ya binadamu pamoja na njaa ya maisha ya kiroho, inayoweza kuzimwa na Yesu Kristo mwenyewe, Mkate wa uzima wa milele.

Maadhimisho ya Kongamano hili la Ekaristi Takatifu yanapania kuwatangazia wananchi wa India Injili ya matumaini, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea ukweli, tayari kushuhudia mwanga katika maisha ya waamini; kwa kuwasaidia maskini na wote wanaoendelea kusukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha, ili wote hawa waweze kuonja upendo wa Kristo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi takatifu.

Katika maadhimisho haya, Kardinali Telesphore Toppo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la ranchi, India ameshirikisha kumbu kumbu ya historia ya maisha yake, pale alipokutana na Mama Theresa wa Calcutta na kumwambia kwamba, Ekaristi Takatifu kwake ilikuwa ni chemchemi ya nguvu katika maisha na utume wake. Hii ndiyo siri ya mafanikio ya utume wa Mama Theresa wa Calcutta katika kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa Mwenyeheri Theresa wa Calcutta kufungua Jumuiya mpya ya kitawa kulimaanisha kuwa n anafasi nyingine tena kwa ajili ya Ibada kwa Ekaristi Takatifu.

Katika maadhimisho ya Kongamano hili, waamini wanaendelea kutoa ushuhuda wa maisha yao na jinsi wanavyoguswa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Tarehe 13 Novemba, 2015 Wakristo kutoka Kandhamal, Orissa watashirikisha ushuhuda wao dhidi ya machafuko ya hali ya hewa yaliyopelekea Wakristo wengi kuuwawa, kunyanyaswa na kudhulumiwa. Lakini, Maaskofu wanasema, hii ni fursa kwa Kanisa Katoliki nchini India kuzama kabisa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni mwaliko kwa waamini kuzama zaidi katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kuwa kweli ni zawadi na sadaka kwa jirani zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.