2015-11-12 09:09:00

Jengeni utamaduni wa huduma ya upendo kwa wagonjwa!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu ya kufungua Mwaka wa masomo wa Kitivo cha tiba na dawa cha Roma, hapo tarehe 11 Novemba 2015 amewataka wanafunzi kuhakikisha kwamba, wanajenga mazingira yatakayowawezesha kudumisha utamaduni wa huduma kwa jirani kwa kutumia vyema karama na mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu. Changamoto hii inahitaji wanafunzi kujiwekea malengo, kwa kuendelea kusoma kwa juhudi, bidii na maarifa, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo!

Kitivo hiki ni matunda ya ugunduzi yaliyofanywa na Mwenyeheri Alvaro Portillo wa Shirika la “Opus Dei”. Hiki ni Chuo kikuu ambacho bado ni kichanga sana nchini Italia na Roma kwa namna ya pekee, lakini ni Chuo ambacho kimekuwa ni rejea kubwa kwa wazazi na walezi kwa ajili ya watoto na vijana wao ili waweze kupata: elimu, ujuzi na maarifa; tayari kuwasaidia wagonjwa wanaoteseka kiroho na kimwili. Anasema, wagonjwa wameonja faraja na upendo kutoka kwenye Jumuiya hii inayojikita katika upendo, ukarimu na mshikamano.

Kardinali Parolin anawataka wanafunzi kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, wanakuwa na ujasiri wa kuweza kufikia malengo wanayojiwekea, kwa kujikita katika ukweli kuhusu maisha ya binadamu. Ukweli huu unafikiwa kwa kusoma kwa juhudi na maarifa; kwa ukarimu na udumifu unaojika katika sadaka binafsi. Wanafunzi wajenge moyo wa unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu anayewakirimia ufahamu wa ukweli wote ambao kimsingi ni Yesu Kristo mwenyewe.

Wanafunzi wanahamasishwa kuwa na Roho wa Mungu anayewajalia nguvu, madaraka na utambulisho wao, tayari kutoka katika ubinafsi wao, ili kushuhudia na kushiriki kikamilifu katika utume wa huduma kwa wagonjwa. Ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, wanatumia akili, ujuzi na maarifa yao yote ili kujenga na kuimarisha mshikamano tayari kuonesha mwanga mahali penye giza, ushuhuda uliotolewa na watakatifu, huo ukawa ni mwanzo wa Pentekoste mpya iliyoleta mageuzi ndani ya jamii kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu pamoja na heshima ya kwa binadamu.

Huu ndio ushuhuda uliotolewa pia na Mtakatifu Josemaria Escrivà de Balaguer aliyekita maisha yake katika sala, ukarimu na huduma kwa jirani kama kielelezo cha utekelezaji wa utume aliopewa wakati wa Ubatizo; dhamana inayojionesha kwa namna ya pekee katika utekelezaji wa majukumu yao kwa weledi kama ushuhuda wa imani tendaji. Kitivo cha tiba na dawa kitoe kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, kwani sayansi inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma ya binadamu na wala si vinginevyo!

Kardinali Pietro Parolin anawataka wanafunzi Chuoni hapo kujenga moyo wa ibada na sala katika maisha yao, kama njia ya kukutana na Yesu anayewakirimia nguvu na ujasiri wa kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo na furaha kwa wagonjwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.