2015-11-12 14:19:00

Imarisheni utume wa familia na vijana; simameni kidete kutetea utu na maisha!


Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 12 Novemba 2015 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia linalofanya hija yake ya kitume mjini Vatican kwa kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya katika shughuli za kichungaji licha ya magumu na changamoto nyingi wanazokabiliana nazo tayari kusoma alama za nyakati. Wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi ni changamoto inayohitaji ushuhuda wa imani tendaji kwa Kanisa kuonesha moyo wa ukarimu, upendo, utu na heshima kwa binadamu mintarafu sheria za kimataifa na kitaifa.

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu wa Slovakia kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, kwa kuheshimiana pamoja na kudumisha utambulisho wa kitamaduni kutoka kwa wananchi wa Slovakia unaojikita katika tunu msingi za maisha ya kimaadili na kiroho; mambo ambayo yanafumbatwa kwa kiasi kikubwa na Mapokeo ya Kanisa Katoliki. Kwa njia hii wanaweza kuchangia katika mchakato wa majadiliano ili kusimama  kidete kulinda na kutetea maisha ya binadamu pamoja na tunu msingi za maisha ya kifamilia.

Ni wajibu wa Kanisa kuonesha dira na mwongozo katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaotumia lugha inayoeleweka kwa waamini wengi, ili ujumbe wa Injili uweze kupenya katika maisha na vipaumbele vya watu, tayari kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu. Waamini walei wawe mstari wa mbele kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya chachu ya kweli za Kiinjili, kwa kuwajengea uwezo wa kujisikia kwamba, hata wao ni sehemu muhimu sana ya Kanisa, ili waweze kutekeleza sera na mikakati mbali mbali ya kichungaji.

Baba Mtakatifu anawapongeza Maaskofu kwa kujifunga kibwebwe kwa ajili ya utume wa familia katika ngazi mbali sanjari na kuwasaidia watoto. Kanisa halina budi kujikita katika utume wa vijana kwa kutambua kwamba, wao ni mbegu ya matumaini kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Wajengewe uwezo wa huduma kwa jirani inayojikita katika mshikamano, ili kukutana na Yesu katika mazingira yao, tayari kumshuhudia; kamwe vijana wasikatishwe tamaa na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali wanazokutana nazo katika maisha. Lakini vijana wanapaswa kufundwa mintarafu mafundisho makini ya Kanisa pamoja na kanuni maadili, ili kujenga mji wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia kuhusu Wakleri amewakumbusha Maaskofu kutoka Slovakia kwamba, hawa ni wasaidizi wao wa kwanza katika maisha na utume wa Kanisa; wanahitaji majiundo makini na endelevu katika masuala ya kitaalimungu, kitasaufi, kichungaji na katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili waweze kuwa kweli ni wainjilishaji waliobobea! Wao ni sura inayowawezesha waamini kukutana na mafumbo ya Kanisa.

Majiundo makini kiroho, kimaadili na kiakili yawe ni chachu ya ushuhuda wa maisha yanayoonesha umoja na mshikamano na Askofu mahalia; udugu na upendo miongoni mwa Wakleri wengine; kwa kuaminiana ili kuwa na amani na utulivu wa ndani; jambo linalowezekana ikiwa kama Wakleri watajenga mahusiano ya karibu na Kristo Yesu. Maaskofu wajenge utamaduni wa kuwasikiliza Wakleri wao kwa moyo wa subira na kuwatendea kwa haki pamoja na kuguswa na mahangaiko yao ambayo wakati mwingine wanakabiliana nayo katika maisha na utume wao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa ni alama na chombo cha umoja miongoni mwa Familia ya Mungu; linapaswa kuwa kweli ni nyumba na shule ya umoja na mshikamano kwa kuheshimiana na kuthamianina kwa kutambua mambo mema na mazuri yaliyoko kwa mwingine, mwelekeo unaopaswa pia kutolewa kwa watawa na watu waliowekwa wakfu katika shughuli za kichungaji. Kanisa nchini Slovakia linaendelea kuhamasishwa kujihusisha na utume miongoni mwa Warom, wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru Maaskofu kutoka Slovakia na kuwaomba wamfikishie salam na matashi mema kwa familia ya Mungu nchini humo, lakini kwa namna ya pekee watawa na makatekista wanaojitaabisha kutangaza na kushuhudia Injili; kwa wale wote wanaotoa huduma ya mapendo na mshikamano kwa maskini na wahitaji na kwamba, wote hawa anawaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa mateso, Msimamizi wa nchi ya Slovakia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.