2015-11-11 14:44:00

Maisha ya pamoja na kielelezo cha Kanisa dogo la nyumbani!


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza rasmi Katekesi yake kwa mahujaji na wageni waliokuwa wamefurika kwa wingi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano tarehe 11 Novemba 2015 amewaalika kusali kwa ajili ya kuombea Kongamano la Kanisa Katoliki Italia linaloendelea Jimbo kuu la Firenze kwa kuwakutanisha: Wakleri, Watawa na Waamini walei ili kupanga sera na mikakati ya shughuli za kichangaji kwa siku za usoni!

Baba Mtakatifu katika Katekesi yake, amekazia umuhimu wa familia kushikamana katika maisha kwa kusali, kula na kushirikishana maisha katika mwanga wa upendo na mshikamano, kielelezo imara cha familia inayopendana. Yesu Kristo aliwaachia wafuasi wake maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kama chakula cha maisha ya kiroho na kwamba, kuna uhusiano wa dhati kati ya familia na Ibada ya Misa Takatifu.

Umoja na mshikamano unaojionesha miongoni mwa wanafamilia unapaswa kuwa ni kielelezo cha Familia kama Kanisa la nyumbani, kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaowakumbatia wote. Kutokana na mwelekeo huu, Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu linakuwa ni alama ya shule ya umoja na mshikamano kati ya waamini, kwa kuwa wasikivu makini kwa mahitaji ya kila mtu. Inasikitisha kuona kwamba, mlo ambalo linapaswa kuwa ni kielelezo cha umoja na mshikamano unapotea katika baadhi ya jamii.

Chakula ambacho ni hitaji msingi la binadamu na kielelezo cha umoja na mshikamano kati ya watu kinaendelea kutupwa ovyo, wakati kuna watu wanaoteseka kwa baa la njaa na utapiamlo. Fumbo la Ekaristi Takatifu liwakumbushe waamini kwamba, wanapaswa kumegeana mkate huu ulioshuka kutoka mbinguni, ili uweze kuwafaidia watu wengi zaidi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, yataziwezesha familia na Kanisa katika ujumla wake kuwa ni alama ya umoja na mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha waamini kwamba, Mwezi Novemba, Mama Kanisa anawakumbuka na kuwaombea kwa namna ya pekee, waamini Marehemu waliolala katika usingizi wa amani, wakiwa na tumaini la maisha ya uzima wa milele. Waamini wawe na ujasiri wa kuboresha maisha yao, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya wanafamilia.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewapongeza wananchi wa Poland wanapoadhimisha Siku kuu ya uhuru wa nchi yao. Mtakatifu Yohane Paulo II  kunako mwaka  1979 aliwakumbusha waamini kwamba, pasi na Yesu Kristo si rahisi sana kuifahamu historia ya Poland. Hii ni changamoto ya kuwa kweli ni waaminifu kwa Injili mintarafu mapokeo ya wahenga wao kwa ajili ya huduma kwa nchi ya Poland.

Ametambua pia uwepo wa Maaskofu Katoliki kutoka Slovakia wanaofanya hija ya kitume mjini Vatican. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, hija hii itawasaidia kuimarisha utambulisho wao kwa Kanisa la Kiulimwengu. Amewataka waamini kuendelea kuwasindikiza Maaskofu wao kwa sala. Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Novemba, linaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Martin wa Tour, mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa upendo na mshikamano kati ya watu na kwamba, hapo mwakani, yaani 2016 Kanisa litaadhimisha Jubilei ya miaka mia moja tangu alipozaliwa, sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa kweli ni wajenzi na vyombo vya huruma ya Mungu na upatanisho; Mwenyezi Mungu aendelee kuwasaidia wagonjwa kuimarisha imani yao hata wakati wanapopambana na majaribu katika maisha. Mwishoni, wanandoa wapya wawe kweli ni chemchemi ya Injili ya furaha kwa kupokea na kukumbatia Injili ya uhai, hususan kwa wanyonge na wasioweza kujilinda wenyewe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.