2015-11-11 07:32:00

Kanisa lipo kati ya watu na kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu!


Yesu alipenda kufahamu jinsi watu walivyokuwa wanamuelewa ili hatimaye, aweze kuwasiliana nao vyema kadiri ya mawazo na misimamo yao ya maisha; katika ukweli na uwazi; wakati wa furaha na majonzi. Kwa Yesu hii ilikuwa ni njia muafaka ya kuweza kuwasaidia, kuwafunda na kuwasiliana nao vyema zaidi, huku wakifungua mioyo yao kusikiliza sauti ya Mungu. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi amejichagulia njia bora zaidi ya kuweza kuwasiliana na binadamu. Jambo hili linawakumbusha Mitume wa Yesu kwamba,  wameteuliwa kati ya watu na kwamba, wao ni sehemu ya jamii.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumanne, tarehe 10 Novemba 2015 wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa michezo wa Luigi Franchi, Jimbo kuu la Firenze katika maadhimisho ya Kongamano la tano la Kikanisa nchini Italia na kuhudhuriwa na bahari ya waamini kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Firenze. Baba Mtakatifu anasema, kwa kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu katika Uwanja wa michezo, kunalikumbusha Kanisa kwamba, linaishi kati ya watu kwa ajili ya watu. Papa Leo mkuu alibeba ndani mwake swali msingi kuhusu utambulisho wa Yesu na akata kuwasaidia watu kumfahamu Kristo Yesu katika undani wa maisha yake.

Swali ambalo Yesu aliwauliza wafuasi wake kuwa watu wanasema kwamba, Yeye ni nani ni muhimu sana kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba anajenga na kukuza imani binafsi kwa Yesu kama sehemu ya utambulisho na utume wao wa Kikristo katika ujumla wao; jambo linalojikita katika ukweli ili kuweza kuona hali halisi ya ubinadamu, ili hatimaye, kuleta utu mpya katika jamii. Kulinda na kutangaza imani ya kweli kuhusu Yesu Kristo ni kiini cha utambulisho wa Mkristo kwani kwa kulifahamu Fumbo la Umwilisho, mwanadamu anaweza kupenya katika Fumbo la Mungu na maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, jibu lililotolewa na Mtakatifu Petro kuhusu utambulisho wa Yesu ni muhtasari wa maisha na utume wake kwa Kanisa kama: mlinzi na mtangazaji wa kweli za imani; kulinda na kuendeleza umoja na mshikamano kwa Makanisa yote sanjari na kutunza nidhamu ya Kanisa. Papa Leo mkuu ambaye Kanisa limeadhimisha Kumbu kumbu yake, hapo tarehe 10 Novemba, ataendelea kuwa ni kielelezo na mfano wa utume huu kwa njia ya unyenyekevu, upendo na nguvu iliyokuwa inatoka kwa Mwenyezi Mungu.

Hata leo hii waamini wanapaswa kuonesha ile furaha kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai, aliyetumwa na Baba, ili aweze kuwa kweli ni chombo cha wokovu kwa binadamu. Huu ni msingi wa imani ya Kikristo, njia ya wokovu na dira ya utimilifu wa maisha ya mwanadamu. Hapa Mwenyezi Mungu anajifunua kuwa ni Mwingi wa huruma na mapendo, aliyejimwilisha, tayari kutambuliwa na watu wake kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro.

Waamini wanaweza kutambua uso wa Yesu katika: Maandiko Matakatifu, Sakramenti za Kanisa; Katika umoja na upendo wa kidugu; Katika huduma na ukarimu kwa wote; kwa kuwaangalia na kuwatunza maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, waamini wamtambue Yesu Kristo aliyeteswa na kufa kifo cha aibu Msalabani. Huu ni ukweli wa kiimani unaojikita katika kashfa ya Yesu kuteswa na hatimaye kufa Msalabani, lakini akainuliwa juu kabisa kuwa ni Bwana wa Ulimwengu.

Huu ndio ukweli ambao hata leo hii unaendelea kusababisha kashfa ya Fumbo la Yesu Kristo. Ni kwa njia ya Fumbo la Msalaba, waamini wanaweza kufahamu, kuungama na kuishi ukweli wa Fumbo la maisha ya Yesu, kwa kujikita katika umoja na mshikamano kati ya watu sanjari na kuambata huruma yake isiyokuwa na kifani! Huu ni mwaliko wa kuendelea kupandikiza mbegu hii katika historia ya maisha ya binadamu, ili hatimaye kuweza kuwa na utu mpya ambao kamwe hauwezi kuwaacha watu wengine pembezoni mwa jamii, au kutowajali katika shida na mahangaiko; bali ni huruma inayojikita katika huduma ya upendo.

Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa kukaza zaidi kwamba, Mungu na binadamu wanategemeana na kutafutana, kwani binadamu anatambua kwamba, ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hii ndiyo hekima ya kweli na kielelezo cha ufuasi wa Kristo, mwaliko wa kuweza kuunganisha: Neno, akili, sala, mafundisho na kumbu kumbu kama anavyohimiza Papa Leo mkuu. Hata leo hii waamini wanaweza kuambata hekima hii kwa kudumisha uhusiano wao na Yesu pamoja na huduma kwa Kanisa. Hapa wanaweza kukutana na binadamu na kuonesha ile sura ya Msamaria mwema na mashuhuda wa upendo kwa Jimbo kuu la Firenze na Italia katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.