2015-11-11 09:35:00

Hija ya maisha ya kiroho inayopania kuimarisha imani!


Kikao cha ishirini cha Taasisi za Kipapa, Jumanne, tarehe 10 Novemba 2015 kimefunguliwa na Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza ka Kipapa la utamaduni na kuhudhuriwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na viongozi waandamizi kutoka Vatican. Kardinali Parolin alisoma ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa ajili ya kikao hiki pamoja na kutoa tuzo kwa washindi binafsi na taasisi zilizojipambanua katika masomo, sanaa pamoja na ukuzaji wa utu wa mwanadamu mintarafu mafundisho ya Kikristo.

Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka huu amemtunuku tuzo Professa Virgilio Lopes kutokana na kampeni ya kutunza makumbusho ya kale, dhamana aliyoifanya katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita: Matteo Bracon kwa kufanya vyema katika masomo yake kwa kutetea sanaa iliyoko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Pudenziana, Jimbo kuu la Roma. Wengine waliopewa tuzo na Baba Mtakatifu ni Almudena Alba Lopez kutoka Chuo Kikuu cha Salamanca, Hispania. Kikao hiki kilifungwa kwa hotuba iliyotolewa na Danilo Mazzoleni, Mkuu wa Taasisi ya Mambo ya kale ya Kikristo na mjumbe wa Taasisi ya Kipapa ya mambo ya kale hapa Roma.

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza wadau mbali mbali ambao wamekuwa mstari wa mbele kuendeleza juhudi zilizoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1995 kwa kuunganisha Taasisi saba za Kipapa ili kuunda Baraza la kuratibu tuzo hii inayotambua mchango wa vijana wa kizazi kipya katika masuala ya elimu, sanaa na hifadhi ya mambo ya kale mintarafu mwendelezo wa utu kadiri ya mafundisho ya Kanisa pamoja na sayansi ya dini.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, vikao vya namna hii ni muhimu sana katika mchakato wa kutajirishana kitamaduni na katika maisha ya ndani, tayari kujenga uwezo wa kupambana na changamoto zinazoendelea kujitokeza ili kuweza kupyaisha utu wa binadamu. Anawashukuru wajumbe kwa kuchagua tema inayogusa hija ya maisha ya kiroho, wakati huu, Mama Kanisa anapojiandaa kuzindua Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, kwa kutambua kwamba, daima mwanadamu ni hujaji katika maisha na kwamba, hata huruma ya Mungu ni lengo ambalo waamini wanapaswa kulipatia kipaumbele cha pekee katika safari ya maisha yao hapa duniani.

Kwa kuvuka lango kuu  la Mwaka Mtakatifu, waamini watahamasishwa kuwa ni vyombo na wajenzi wa huruma ya Mungu katika maisha yao, wakijitahidi kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni. Mada hii inaonesha umuhimu wa waamini kufanya hija katika maeneo mbali mbali ya kihistoria, maisha na utume wa Kanisa. Hija ni kielelezo cha ujasiri na sadaka ya kutaka kuzima kiu ya kutaka kukutana na mashuhuda wa imani, ili kujenga na kuimarisha imani, matumaini na huruma. Ni changamoto ya kukuza ukarimu unaojionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu ni mwaliko kwa waamini kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa wageni; kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya furaha. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu iwe ni fursa kwa Makanisa mahalia kuweza kujizatiti zaidi katika kutekeleza malengo ya maisha na utume wake. Iwe ni fursa ya waamini kukutana na Kristo Yesu pamoja na ndugu zao katika imani. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua nafasi huu kuwashukuru na kuwatia shime wale wote wanaopania kuchangia kwa hali na mali katika kufanikisha hija za maisha ya kiroho katika maeneo mbali mbali ya kihistoria. Mwishoni, anawapongeza wote walioshinda tuzo ya Kipapa kwa mwaka 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.