2015-11-11 15:57:00

Familia isiyojishikamanisha na Mungu, iko siku itabwaga manyanga!


Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha baadhi ya changamoto zilizojadiliwa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia iliyohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, Sinodi hii ilikuwa ikiongozwa na kauli mbiu wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo.

Askofu Ngalalekumtwa anasema wanadoa watarajiwa wasipofanya maamuzi magumu katika hali ya ukomavu na busara; utulivu na amani ya ndani, kuna hatari ya kuanza kuchokana mapema na huo ukawa ni mwanzo wa kuvunjika kwa maisha ya ndoa na familia. Wanandoa watarajiwa wakumbuke kwamba, huu ni wito na maisha yanayomwambata Kristo, ili aweze kuwafunda na kuwaelekeza katika safari ya maisha, tayari kukumbatia Injili ya maisha, imani na matumaini. Watambue kwamba, uzuri wa nje ni mapambo mpito na badala yake wajikite katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, hadi kifo kitakapowatenganisha.

Vijana wakikimbilia na kukumbatia mambo ya nje, kuna hatari ya kukengeuka na kutumbukia katika “nyumba ndogo”, “vidumu” au kukimbilia “chocho” hatari kwa maisha ya ndoa na familia! Wanandoa wanatarajiwa kuwa kweli mwili mmoja na roho moja katika maisha yao.

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa anasema, kuvunjika kwa maisha ya ndoa na familia kunasababishwa na mambo mengi: kushamiri kwa ndoa za mkeka pasi na maandalizi ya kutosha. Pili viongozi wa Kanisa kutowapatia wanandoa watarajia mafundisho muhimu na endelevu katika safari ya ndoa na familia, ili kuweza kufahamiana kiutu; kiimani, kimsimamo na kama kweli wataweza kuishi kwa pamoja maisha yao yote!. Maandalizi hafifu yanayotolewa kwa wanandoa ni sababu kubwa inayopelekea wanandoa wengi kujikuta wakiwa njia panda.

Askofu Ngalalekumtwa ambaye amehudhuria Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia katika awamu zote mbili anakaza kusema, udhaifu wa kibinadamu, tamaa za mwili, ukosefu wa uaminifu katika maisha ya ndoa ni sababu nyingine zinazopelekea ndoa nyingi kuvunjika. Wakati mwingine matatizo ya kiuchumi yamechangia kwa kiasi kikubwa kuvunjika kwa ndoa, kwani pengine hakukuwepo na upendo wa dhati, lakini kilichopendwa ni pochi! Myumbo wa uchumi unapotikisa familia, baadhi ya watu wanashindwa kuvumilia na matokeo yake ni kubwaga manyanga! Familia isiyojishikamanisha na Mungu kwa njia ya Sala, Sakramenti za Kanisa na Neno la Mungu, hiyo iko hatarini kusambaratika. Waamini wajenge utamaduni wa kumchokoza Mungu kwa njia ya sala na tafakari ya Neno la Mungu, vinginevyo maisha yatapooza kama supu ya makongoro ya ng’ombe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.