2015-11-10 09:16:00

Waamini shuhudieni tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kumwabata Kristo!


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limeanza maadhimisho ya Kongamano la tano la Kikanisa kwa kuwataka waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa imani tendaji inayojikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji na ari ya kimissionari katika maisha na utume wa Kanisa nchini Italia katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo! Jambo la msingi ni ushuhuda wa maisha ya Kikristo kwa kuambata utu mpya kutoka kwa Kristo.

Huu ni mwaliko wa kuendeleza utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, tayari kujikita katika azma ya Uinjilishaji mpya, kwa kuwashirikisha na kuwamegea wengine ile furaha na matumaini ya kukutana na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Hii ni furaha inayobubujika kutoka katika Neno la Mungu, maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa pamoja ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo katika medani mbali mbali za maisha.

Ushuhuda wa imani, maadili na utu wema ni mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa anasema Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino katika hotuba yake ya ufunguzi, Jumatatu tarehe 9 Novemba 2015 huko Jimbo kuu la Firenze. Maadhimisho ya kongamano hili yanajikita katika mtindo wa kisinodi, unaopaswa kuwa sasa ni dira na mwongozo kwa Jumuiya za Kikristo.

Makongamano ya Makanisa mahalia nchini Italia anasema Askofu mkuu Nosiglia, hayana budi kusikiliza kilio cha binadamu wanaoteseka; kwa kuambata mambo msingi katika maisha; tayari kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha; maskini na wote wanaoendelea kusukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa bila kusahau changamoto ya elimu na malezi kwa vijana wa kizazi kipya.

Mikutano na majadiliano yote haya yalenge kujenga na kuimarisha utamaduni wa watu kukutana jambo linalokaziwa sana na Baba Mtakatifu Francisko. Kongamano hili linapenda pamoja na mambo mengine kukazia umuhimu wa Kanisa kutoka, kutangaza, kuishi, kufundisha na kubadilisha kwa kujikita katika mambo msingi katika maisha ya waamini. Kongamano hili ni mwendelezo wa Kongamano lililofanyika Jimbo kuu la Verona kunako mwaka 2006.

Kwa upande wake, Kardinali Giuseppe Betori, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Firenze, katika hotuba yake amependa kwa namna ya pekee kabisa kuwakaribisha wajumbe wa kongamano hili kutoka sehemu mbali mbali za Italia, waliokusanyika kwenye Kanisa kuu baada ya maandamano kutoka katika Makanisa jirani. Firenze ni mji ambao unahistoria kubwa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, uzuri wa utamaduni na sanaa; kwa kuwasaidia na kuwahudumia wagonjwa, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wote waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Ni mji unaonesha kwa ufupi mambo msingi yanayopaswa kukumbatiwa na waamini katika hija ya maisha yao ya kiroho, kwa kutafuta kilicho chema, kizuri na kitakatifu, ili kweli kuweza kumwilisha Injili ya upendo kwa Familia ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.