2015-11-10 08:17:00

Jubilei ya miaka 50 ya wito na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa!


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wao juu ya utume wa waamini walei, uliopitishwa kunako tarehe 18 Novemba 1965 wanabainisha kwa kina na mapana kuhusu: Wito wa waamini walei kwa kazi ya kitume; madhumuni ya utume wa walei katika mchakato wa Uinjilishaji na kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya imani tendaji inayojikita katika matendo ya huruma; nyanja mbali mbali za utume wa walei miongoni mwa familia, vijana, mazingira ya kijamii; katika masuala ya kitaifa na kimataifa.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanaangalia pia aina mbali mbali za utume wa waamini walei, utaratibu unaopaswa kufuatwa ili kujenga mahusiano mema na viongozi wa Kanisa; vyombo vya ushirikiano katika kukuza na kuendeleza majadiliano ya kiekumene pamoja na umuhimu wa kuwajengea waamini walei uwezo katika medani mbali mbali za maisha, ili waweze kutekeleza dhamana yao kikamilifu.

Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kuchapishwa kwa Waraka juu ya utume wa waamini walei unaojukulikana kama “Apostolicam actuositatem”, Jumanne tarehe 10 Novemba 2015 kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Santa Croce kilicho hapa mjini Roma, Baraza la Kipapa la waamini walei, linapenda kwa mara nyingine tena kupembua kwa kina na mapana wito na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa na katika ulimwengu kwa kufanya kongamano ambalo linawashirikisha viongozi wakuu wa Baraza la kipapa la waamini walei pamoja na wasomi mbali mbali, ili kuangalia wito na utume wa waamini walei tangu baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican hadi wakati huu.

Wanajadili pamoja na mambo mengine kuhusu changamoto zinazowakabili walei katika ulimwengu mamboleo katika masuala ya: familia, elimu, mapambano dhidi ya umaskini na jitihada za kusimama kidete kwa ajili ya mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.