2015-11-09 10:28:00

Safari ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani inaendelea!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo! Karibu tuendelee kukitegea sikio kipindi chetu pendevu sana cha hazina yetu. Baada ya kusafiri umbali wa kutosha na ule waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko katika kutuandaa kuuadhimisha mwaka wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu, leo tunapenda kurudi kwenye mada nyingine ambayo tunatembea nayo katika mwaka huu; nayo si nyingine bali ni maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.

Tutakumbuka kwamba, kabla ya Baba Mtakatifu kuweka nia ya kuitangaza Jubilei kuu ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, tulikuwa tumekishaanza maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Mwaka huo wa watawa ulizinduliwa rasmi tarehe 30 Novemba 2014 na utahitimishwa rasmi tarehe 2 Februari 2016, katika Sherehe ya kutolewa Bwana Hekaluni, ambayo kimsingi ni Siku ya Watawa Duniani.

Katika hati yake ya kuuzindua mwaka huu wa watawa, Baba Mtakatifu Francisko anawapatia watawa malengo makuu matatu. Kwanza kabisa Baba Mtakatifu anawaalika watawa kuishukuru historia iliyopita; na pili anawaalika watawa kuishi sasa katika ukamilifu wote; tatu na mwisho anawaalika watawa kukumbatia wakati ujao kwa matumaini makubwa. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu analialika kila shirika la kitawa na taasisi ya maisha ya kitume, kuelewa vyema Karama yao, na kujichunguza kama kweli Kristo bado ni upendo wao wa kwanza na wa mwisho, au wamebadili mwelekeo.

Baba Mtakatifu anasema, katika Mwaka huu wa watawa, watawa wote waume kwa wake, wauamshe ulimwengu, wao wenyewe wawe na furaha timilifu na daima tayari kutoa majibu sahihi kwa changamoto zinazoikabili jamii ya mwanadamu wa leo. Katika hili anaongeza kwamba, ‘watawa wafikiri namna gani wanaweza kuwasaidia Wakristo wanaodhulumiwa sehemu mbali mbali duniani. Na mwisho kabisa Baba Mtakatifu, katika mwaka huu wa watawa anategemea mashirika ya kitawa na taasisi za maisha ya kitume zinaweza kujileta karibu zaidi na zaidi. Kwa upande wa waamini walei, Baba Mtakatifu anawaomba wayajali maisha ya uwakfu na wawaheshimu watawa.

Kuusindikiza Mwaka huo wa Watawa Duniani, Baba Mtakatifu Fransisko aliandika barua rasmi kwa wote wenye kuyaambata maisha ya uwakfu. Kipande cha Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa watawa katika Mwaka huu wa Maisha ya Wakfu kinasema hivi:

Wapendwa kaka na dada katika maisha ya kitawa,

Ninawaandikia barua hii kama mrithi wa Mtume Petro, ambaye Bwana alimpa jukumu la kuwaimarisha ndugu zake katika imani (rej. Lk 22:32). Lakini pia ninawaandikia ninyi kama kaka yenu, ambaye kama ninyi wenyewe, nami nimejiweka wakfu kwa Mungu. Kwa pamoja, tumshukuru Mungu, ambaye ametuita kumfuasa Yesu kwa kuiambata Injili na kulitumikia Kanisa, kwa nguvu na msaada wa Roho yule aliyemiminwa katika mioyo yetu. Kufuatia maombi mengi niliyoyapata kutoka kwa wengi wenu, na kutoka kwa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume, nimeamua kuutangaza huu mwaka wa Maisha ya Wakfu, katika nafasi ya Maadhimisho ya Miaka 50 tangu kuandikwa kwa Katiba ya Kikanisa “Mwanga wa Mataifa, ambayo katika sura ya 6 inaongelea juu ya Watawa; na pia tangu kuandikwa ile hati ya “Perfectae Caritatis” yaani Mapendo Kamili, ambayo inahusu upyaishwaji wa maisha ya Wakfu”.

Baada ya kuwasiliana Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume nimechagua malengo ya Mwaka huu kuwa ni haya yafuatayo: Kuutazama wakati ulopita kwa shukrani: Taasisi zote za kitawa, zinabeba historia nzito iliyojaa utajiri wa karama mbalimbali. Mwanzoni mwa kila shirika, tunaona Mkono wa Mungu, ambao kwa njia ya roho wake huwaita baadhi ya watu kumfuasa Kristo kwa karibu zaidi, kutafsiri Injili kwa namna ya pekee, kusoma ishara za nyakati kwa macho ya imani, na kwa njia ya ubunifu kujibu mahitaji ya Kanisa ya wakati huo.

Katika mwaka huu wa watawa, ingekuwa ni vema sana kwa kila Shirika la kitawa kutafakari mwanzo wake na historia yake, ili kuweza kumshukuru Mungu anayelijalia Kanisa Karama mbalimbali ambazo zinaling’arisha na kuliwezesha kwa ajili ya kazi njema yaani utume.  (Rej. Mwanga wa Mataifa, 12). Ni mwaliko kwa watawa, kila shirika kuitafakari historia yao kwa ajili ya kutunza hadhi yao, kuimarisha umoja wa kishirika kama familia na kukuza  uzalendo wa kila mtawa kwa shirika. Kutafakari historia kunawaalika wataka kama shirika na kama mtawa mmoja mmoja pia, kufuata nyayo za vizazi vilivyopita ili kung’amua tunu kuu za maisha, pamoja na mitazamo na vitu vilivyowaangaza waanzilishi wa mashirika mbalimbali hata wakaanzisha jumuiya za kitawa.

Ni kwa namna hiyo, kila shirika litaona, ni namna gani Karama ya shirika imemwilishwa kwa miaka iliyopita, ubunifu uliokuwepo, magumu yaliyokuwepo na namna halisia walizozitumia katika kutatua changamoto na magumu hayo. Baba Mtakatifu anasema “Kuitazama na kuisimulia historia kama watawa katika shirika, ni kumtukuza Mungu na kumshukuru kwa kwa mapaji yote aliyotujalia”.

Mwaka huu wa watawa, iwe ni nafasi ya kuungama imani kwa unyenyekevu  na matumaini kwa Mungu ambaye ni upendo (1Yh 4:8). Na pia ni kipindi cha kutubu makosa yetu kama watawa na hivyo kuonja upendo wa huruma ya Bwana. Ni wakati pia wa kudhihirisha kwa ulimwengu furaha yetu katika kumfuasa Kristo katika maisha haya ya wakfu. Lengo la pili la maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, ni mwaliko kwa watawa wote kuishi sasa kwa ukamilifu wote. Anafafanua  Baba Mtakatifu; Kumbukumbu ya yaliyopita, kwa msaada wa Roho Mtakatifu inatuongoza kuyatekeleza kwa ukamilifu zaidi yale mambo msingi ya maisha ya uwakfu. Roho wa Mungu daima amewaongoza watu kumfuasa Kristo kama Injili inavyoagiza.

Ni kwa sababu hiyo, anasema Baba Mtakatifu, waanzilishi wengi wa Mashirika, walikuwa na Injili kama sheria msingi. Na sheria na Kanuni nyinginezo zote vilikuwa ni vielelezo vinavyoelezea zaidi Injili na namna ya kuishi Injili kwa ukamilifu. Kwao kioo na mfano alikuwa ni Yesu Kristo mwenye ambaye walitamani kumfuasa, na kuungana naye kabisa, hata wakatamani kusema pamoja na Mtume Paulo “kwangu mimi kuishi ni Kristo (Fil. 1:21). Nadhiri zao zilikuwa ni alama wazi ya mapendo yao kwa Kristo.

Mpendwa Msikilizaji, tunapoelekea ukingoni mwa maadhimisho ya Mwaka wa watawa duniani, tutakuletea makala zinazohusu maisha ya kitawa, historia yake na utofauti wake. Tutakubaliana na ukweli kwamba, kila pahali duniani, kila huyo kwa namna yake, tumewahi kuguswa kwa namna ya pekee na uwepo na huduma ya watawa. Kumbe ni mwaliko kwetu sote kuendelea kuwasindikiza watawa wetu kwa sala na majitole yetu, na kama anavyotualika Baba Mtakatifu, sote kabisa tushukuru uwepo wa Maisha ya kitawa katika Kanisa; na tuwashukuru sana watawa kwa maneno na matendo, tuwape shime na ushirikiano mwema, tuwaundie mazingira mazuri na salama ili waendelee kutumegea upendo wa Kristo kwa njia ya uwepo wao na huduma zao kwetu.

Kukuletea makala hii kutoka katika Hazina yetu, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB, mtawa wa Shirika la Mtakatifu Benedikto.








All the contents on this site are copyrighted ©.