2015-11-09 09:31:00

Radio Maria inapania kukuza na kudumisha moyo wa sala na ibada!


Padre John Maendeleo Mkurugenzi wa Radio Maria Tanzania ni kati ya viongozi wakuu wa Radio Maria waliohudhuria mkutano mkuu wa Radio Maria uliofanyika huko Collevalenza, nchini Italia kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 30 Oktoba 2015. Mkutano huu uliwashikirisha Mapadre na Wakurugenzi wa Radio Maria, ili kupembua kwa kina na mapana kuhusu karama ya Radio Maria pamoja na kupanga sera na mikakati itakayotekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Padre John Maendeleo anasema, Radio Maria inaendelea kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, chini ya usimamizi, maongozi na tunza ya Bikira Maria. Radio Maria inapenda kujikabidhi chini ya Bikira Maria katika maisha na utume wake, ili kweli Bikira Maria aweze kuwasaidia katika mchakato wa Uinjilishaji. Katika mkutano mkutano mkuu, viongozi wa Radio Maria wamejadili mikakati ya kuiwezesha kufikisha ujumbe wake kwa watu pamoja na watu wenyewe kushiriki kikamilifu kuchangia maisha na utume wa Radio Maria kwa hali na mali.

Kwa njia hii, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanashiriki katika mchakato wa Uinjilishaji, dhamana inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Radio Maria inapania kuwajengea watu moyo wa Sala na Ibada; kama sehemu ya mchakato wa watu kukutana na Muumba wao. Dhamana hii imepewa uzito wa pekee wakati wa mkutano wa viongozi wakuu wa Radio Maria.

Padre John Maendeleo anakaza kusema, walipata pia nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican aliyekazia kwa namna ya pekee karama ya Radio Maria katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Amesema kwamba, Radio Maria imekuwa ni mdau mkuu katika azma ya Uinjilishaji, kwa kugusa mahangaiko ya watu, tayari kuwatangazia Injili ya furaha, matumaini, mapendo na huruma inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa lake.

Baba Mtakatifu ameipongeza Radio Maria kwa kujiaminisha mbele ya Mungu kiasi kwamba, daima imefanikiwa kutekeleza mikakati yake ya Uinjilishaji, kwa kuwagusa watu na watu wenyewe kuchangia kwa hali na mali. Baba Mtakatifu anaitaka Radio Maria kuwa aminifu kwa Injili na Mafundisho ya Kanisa. Isaidie kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, moyo wa sala na liturujia.

Padre John Maendeleo anasema, katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, Radio Maria inapenda kuzindua Radio sita katika maeneo mbali mbali ya Bara la Afrika, ili kuliwezesha Kanisa kuwafikia watu wengi zaidi. Ni wakati wa kukazia moyo wa: Sala; Maisha adili na matakatifu, ili kuwawezesha waamini kutambua uwepo wa Mungu na maisha ya uzima wa milele. Watu wawe wajiandaye kwa ajili ya kushiriki maisha baada ya kifo kwa kuendelea kuambata maisha ya kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.