2015-11-09 08:36:00

Jivikeni utu mpya kwa kumwambata Yesu Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha!


Askofu Franco Agostinelli wa Jimbo Katoliki Prato anasema, Familia ya Mungu Jimboni humo inamsubiri kwa hamu Baba Mtakatifu Francisko anapowatembelea, akiwa njiani kuelekea Jimbo kuu la Firenze kwenye maadhimisho ya Kongamano la tano la kitaifa nchini Italia. Hili ni tukio ambalo linawaimarisha katika imani, matumaini na mapendo kwa kutambua kwamba, Baba Mtakatifu anaguswa na mahangaiko ya watu wengi kutokana na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa.

Baba Mtakatifu anatambua fika juu ya ukosefu wa fursa za ajira na jinsi ambavyo familia nyingi zinaendelea kutumbukia katika lindi la umaskini wa hali na kipato kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Ndiyo maana Baba Mtakatifu akiwa Jimboni Prato anataka kuzungumza na wafanyakazi kwani mji wa Prato unajipambanua kwa kazi na unaendelea kujengwa kwa jasho la wafanyakazi. Lakini kwa wakati huu, kuna wananchi wengi ambao hawana fursa za ajira na wanaendelea kuogelea katika hali ngumu ya maisha.

Wafanyakazi wanasubiri kwa hamu neno kutoka kwa Baba Mtakatifu, ili kuwatia shime katika shida na mahangaiko yao. Lakini kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wataendelea kuimarishwa katika ushuhuda unaojikita kwenye ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi ili wote waweze kujisikia kuwa kweli wanakubalika na kupokelewa kama watoto wa Mungu.

Jimbo Katoliki la Prato linapaswa kuwa kweli ni maabara ya ukarimu, umoja na mshikamano kati ya watu, ili kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana kwa amani na utulivu. Hapa kuna idadi kubwa ya wananchi kutoka China wanaojihusisha na biashara. Itakuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza nao, tayari kwa Jimbo Katoliki Prato kujielekeza zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Kwa upande wake, Kardinali Giuseppe Betori, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Firenze anasema, Familia ya Mungu Jimboni humo inataka kumpokea Papa Francisko kama Baba wa wote na mchungaji mkuu wa Kanisa Katoliki. Waamini wanataka kumwonesha moyo wa ushirikiano na mshikamano katika utekelezaji wa dhamana na wito wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Hii ni fursa kwa Baba Mtakatifu kukutana walau kwa kiasi kikubwa na Familia ya Mungu Jimbo kuu la Firenze, lakini kwa namna ya pekee, atapata nafasi ya kusali pamoja na wagonjwa sanjari na kupata chakula cha mchana na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Familia ya Mungu Jimbo kuu la Firenze inatambua kwamba, Baba Mtakatifu anawapenda na kuwathamini; anatambua shida na mahangaiko yao ya ndani na kwa sasa anataka kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo, tayari kumshuhudia Kristo kwa njia ya imani inayomwilishwa katika matendo!

Kongamano hili la Kikanisa nchini Italia ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kugundua ndani mwao utu mpya wanaojivika kwa njia ya Yesu Kristo, chemchemi ya matumaini mapya katika shida na mahangaiko yao. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kuwa kweli waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake kwa kutunza na kudumisha ile sura na mfano wa Mungu ndani mwao. Wakristo wawe ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na ukarimu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kujikita katika Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.