2015-11-09 08:19:00

Jifunzeni moyo wa ukarimu na sadaka kutoka kwa shule ya Mama mjane!


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya thelathini na mbili, hususan Injili, inaangalisha juu ya mambo makuu mawili ambayo Wakristo wanapaswa kuyazingatia: kwanza kabisa ni kuachana na mfano na maisha ya Wafarisayo waliokuwa wanapenda heshima mbele ya watu, lakini ndani mwao walificha uovu na ukosefu wa misingi ya haki, wakala kwenye nyumba za wajane na kushindwa kuwatetea yatima na wageni. Sala ya kweli inamwilishwa katika haki, kwani haiwezekani kuwa na Ibada ya kweli kwa Mwenyezi Mungu wakati huo huo, ukiwanyanyasa na kuwadhulumu maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 8 Novemba 2015. Baba Mtakatifu anasema, Wakristo wanapaswa kuiga mfano wa Mwanamke mjane aliyejitosa bila ya kujibakiza, kiasi cha kutoa senti ya mwisho aliyokuwa nayo, ikilinganishwa na matajiri waliokuwa wanatoa fedha zilizokuwa zimewazidi.

Yesu anamwangalia mwanamke mjane kwa jicho la upendo na kumpongeza kwani alikuwa ametoa zaidi kuliko wengine wote. Katika umaskini wake anasema Baba Mtakatifu, mwanamke mjane ametambua kwamba, kweli anapendwa na Mwenyezi Mungu na kuamua kurudisha upendo huu kwa njia ya ukarimu uliokuwa unabubujika kutoka moyoni mwake. Kinachotakiwa hapa si wingi wa fedha na sadaka inayotolewa, bali kile kinachobubujika kutoka moyoni kwa ukarimu kama kielelezo cha utimilifu wote na hivyo kushinda kishawishi cha kung’ang’ania sana fedha kiasi hata cha kushindwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani.

Kumpenda Mungu kwa moyo wako wote ni kielelezo cha mwamini kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kumtumikia kwa njia ya maskini bila kutegemea kurudishiwa chochote kile! Baba Mtakatifu Francisko anasema, upendo wa kweli unajikita katika matendo kwa kutoa mambo msingi na wala si kile kinachozidi. Ili kujibu kilio cha maskini, kuna haja kwa waamini kujinyima mambo msingi kwa ajili ya wengine. Sadaka hii inaweza kuwa ni: muda, karama na vipaji ambavyo mwamini amekirimiwa na Mwenyezi Mungu.

Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza ukarimu kutoka kwenye shule ya mwanamke mjane aliyeyamimina maisha yake yote kwa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu. Mwanamke huyu ananyanyuliwa juu na kupewa heshima ya pekee na Yesu, kama kielelezo cha Injili hai, mwaliko kwa waamini kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwaombea kwa Mwanaye wa pekee moyo wa umaskini, lakini unaosheheni utajiri wa ukarimu na majitoleo bila ya kujibakiza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.