2015-11-09 09:52:00

Hakuna mapya chini ya anga! Yote yanaeleweka! Ukweli, uwazi na maadili muhimu


Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linaweza kufanya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wake kwa kuambata kwanza kabisa maisha ya sala na utakatifu wa maisha, kama cheche za kuyatakatifuza malimwengu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kuiba nyaraka za siri kutoka Vatican ni kitendo cha jinai na wala hakina masilahi kwa ustawi na maendeleo ya Kanisa. Baba Mtakatifu pamoja na wasaidizi wake, wataendeleza mchakato wa kuleta mageuzi ndani ya Kanisa kwa kuzingatia ukweli na uwazi.

Matukio kama haya yanaposikika masikioni mwa waamini na watu wenye mapenzi mema, yanakera na kutibua nyongo za watu! Inasikitisha kuona kwamba, Padre anasaliti maisha, wito, dhamana na imani ambayo alikuwa ameoneshwa na Baba Mtakatifu Francisko. Jambo hili linasikitisha sana, lakini, Baba Mtakatifu anaendelea kusonga mbele kwani ndani mwake anayo nguvu ya kimaadili na anatambua kwamba, kuna watu wanaomsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka zao!

Huu ni mfano bora wa kuigwa na viongozi wa Kanisa pamoja na wale wote waliokabidhiwa dhamana ya kuonesha njia na dira katika maisha ya watu wanaowazunguka. Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani kwa kujikita katika mambo muhimu ya maisha na kwamba, wafanyakazi wa Vatican wanapaswa kuonesha ukomavu katika maadili, ukweli na uwazi. Hii ni sehemu ya mchakato wa mageuzi yanayoendelea kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko na matunda ya kazi hii nyeti, ngumu na endelevu yanaendelea kujionesha.

Haya yamesemwa na Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha TV2000 kinachomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuhusiana na uvujishaji wa nyaraka za siri kutoka Vatican na hatimaye, kuchapishwa katika vitabu viwili, jambo ambalo ni kosa la jinai. Askofu mkuu Becciu anasema, yale yote yaliyochapishwa kwenye vitabu hivi ni mambo ambayo tayari yalikuwa yanafahamika na viongozi wakuu wa Vatican na yalikwisha fanyiwa kazi na matunda yake yameanza kuonekana. Waamini wanapochangia kwa hali na mali katika Mfuko wa Mtakatifu Petro wanatambua kwamba, wanataka kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuliongoza Kanisa, fedha ambayo inatumika katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kiulimwengu na kwenye Makanisa mahalia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.