2015-11-07 11:57:00

Kampeni za uchaguzi nchini Uganda zaanza kutimua vumbi!


Rais Yoweri Kaguta Museveni tayari amezindua Ilani ya chama chake na tayari kampeni za Urais na wabunge zimeanza kupamba moto nchini Uganda. Taarifa zinaonesha kwamba, Uganda itafanya uchaguzi mkuu hapo tarehe 18 Februari 2016. Haya yamesemwa na Tume ya Uchaguzi Nchini Uganda. Hadi sasa kuna wagombea nane wa kiti cha Urais nchini Uganda, wakiongozwa na nguri wa siasa nchini Uganda, Rais Museveni, ambaye ameiongoza Uganda kwa takribani miaka 29.

Vyama vya upinzani vinaongozwa na Dr. Kizza Besigye, aliyewahi kuwa daktari binafsi wa Rais Museveni, na kwa miaka mingi amekuwa akimsumbua Rais Museveni katika chaguzi kadhaa zilizopita. Ni kiongozi anayewakilisha Jukwaa la mageuzi kwa ajili ya Uganda akifuatiwa na Amama Mbabazi aliyekuwa Waziri mkuu kwenye Serikali ya Rais Museveni, lakini amejiengua na kuingia kwenye kambi ya upinzani. Taarifa zinaonesha kwamba, Wakili Faith Kyalya ndiye mwanamke pekee aliyejitosa kimasomaso kuwania kiti cha Urais nchini Uganda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.