2015-11-06 09:15:00

Wafungwa walioachiwa huru waoneshe mfano bora katika jamii!


Jela ni mahali ambapo mtu anapaswa kusaidiwa ili kujirekebisha na baada ya kumaliza muda wake wa kifungo, aweze kurejea tena katika jamii kuendelea na maisha bora zaidi, kwa kuonesha kwamba, adhabu aliyoitumikia akiwa kifungoni imemsaidia kuwa mtu mwema zaidi. Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa 4,160 ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuaga na kumpisha mrithi wake, Rais Dk. John Magufuli. Kati ya wafungwa hao, 864 wameachiwa huru na 3,293 kupunguziwa vifungo vyao na kubaki gerezani wakitumikia sehemu iliyobaki ya kifungo chao. Taarifa ya Serikali ya awamu ya tano imetolewa Alhamisi tarehe 5 Novemba 2015 na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, ilieleza kuwa, Kikwete alitumia madaraka aliyopewa chini ya ibara ya 45 (1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Ni mategemeo ya serikali kwamba wafungwa watakaochiwa huru watarejea katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa taifa na watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo. Taarifa hiyo ilisema wafungwa wote wapunguziwe moja ya sita ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58. Pia ilieleza kuwa msamaha huo utawahusu wafungwa wenye magonjwa kama upungufu wa kinga mwilini (Ukimwi), kifua kikuu na saratani ambao wako katika hali mbaya kwa kuthibitishwa na jopo la madaktari chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya. Ilisema msamaha huo utawahusu wafungwa wenye umri wa kuanzia miaka70 na kuendelea. Kundi lingine la msamaha litawahusu wafungwa wa kike waliongia gerezani wakiwa na ujauzito pamoja na wanawake waliongia gerezani na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

Kadhalika, msahama huo utawahusu wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili uliothibitishwa pia na jopo la waganga. Hata hivyo, msamaha huo hautawahusu wafungwa wenye makosa makubwa kama waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa, waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani, waliojihusisha na usafirishaji na matumizi ya dawa za kulenya, waliohukumiwa kujihusisha na uombaji, upokeaji au utoaji rushwa.

Wengine wasionufaika na msamaha huo ni wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kupatikana na silaha, risasi au milipuko isiyo halali, kunajisi, kubaka, kulawiti, kuwapa mimba wanafunzi, makosa ya wizi wa magari na pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo na wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole na Sheria ya Huduma kwa Jamii.

Wengine ni waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao, waliowahi kupunguziwa kifungo na msamaha wa Rais na bado wangali wakiendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki, wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka wakiwa chini ya ulinzi, wanaotumika vifungo kwa makosa ya wizi au ubadhirifu wa fedha serikalini, wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji wa nyara za serikali na ujangili, waliohukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu pamoja na vitendo vya mashambulizi na ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Na mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.