2015-11-06 10:40:00

Sakramenti ya Upatanisho ipewe kipaumbele cha kwanza wakati wa Jubilei


Iweni na huruma kama Baba Yenu wa Mbinguni ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu itakayozinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2015 wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili. Bikira Maria ni shuhuda amini wa huruma ya Mungu iliyofanyika mwili,yaani Yesu Kristo, ikamwezesha kuingia katika Hekalu la huruma ya kimungu kwa sababu aliliishi kwa dhati Fumbo la upendo wa Mungu.

Bikira Maria alibahatika kuwa kweli ni Sanduku la Agano na shuhuda wa huruma ya Mungu pale chini ya Msalaba, huruma inayoweza kuwakumbatia na kuwafumbata wote pasi na ukomo! Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu ni kipindi cha hija ya maisha ya kiroho kama ile aliyofanya Bikira Maria kwa kumtembelea binadamu yake Elizabeth. Hija hizi zisaidie mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwawezesha waamini kupata rehema inayotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Hija hizi ziwasaidie waamini kushikamana na huruma ya Mungu, tayari kuwamegea wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku, kwa kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa huruma ya Mungu duniani. Mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanatarajiwa kutembelea Nchi Takatifu mahali alipoazaliwa, alipoteswa na kufariki dunia Kristo Yesu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki Nchi Takatifu katika mkutano wao uliokuwa unafanyika kuanzia tarehe 3 hadi tarehe 5 Novemba, wanawataka Mapadre kuhakikisha kwamba, wanawasaidia waamini kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.

Lengo ni kuwawezesha waamini kufaidika zaidi na rehema na neema inayotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Mahujaji wanahimizwa kuhakikisha kwamba, katika mipango na mikakati yao wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu, wahakikishe kwamba, wanakuwa na ratiba ya kupokea Sakramenti ya Upatanisho na kwamba, Madhabahu pamoja na Makanisa mbali mbali yahakikishe kwamba, panakuwepo na Mapadre wa kutosha ili kutoa Sakramenti ya Upatanisho kwa wale watakaokuwa wanakimbilia huruma na upendo wa Mungu.

Katika mkutano wa viongozi wakuu wa Kanisa huko Nchi Takatifu, wamepembua kwa kina na mapana utume unaotekelezwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki mjini Yerusalemu, Caritas Yerusalemu kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na kuangalia miradi mbali mbali ambayo imetekelezwa kwenye Ukanda wa Ghaza. Maaskofu wanawataka viongozi wa Makanisa mahalia kuhakikisha kwamba, wanaanzisha tume itakayowasaidia maskini katika Parokia mbali mbali kwa kushirikiana na Caritas Yerusalemu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.