2015-11-06 09:56:00

Mwanasheria mkuu George Mcheche Masaju, Kikao cha Bunge 17 Nov; Waziri mkuu?


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ameanza kazi kwa kasi na kishindo kikuu ambapo Alhamisi tarehe 5 Novemba 2015 kwa kumteua Mwanasheria mkuu wa Tanzania pamoja na kuitisha kikao cha kumi na moja cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Changamoto kubwa iliyoko nchini Tanzania kwa sasa ni pamoja na kura ya maoni, iliyohailishwa ili kutoa nafasi kufanyika kwa uchaguzi mkuu pamoja na uchaguzi wa marudio Visiwani Zanzibar, ili kweli haki, amani na maridhiano viweze kutawala tena miongoni mwa watanzania.

Akizungumza na waandishi wa Habari kwa niaba ya serikali katika viwanja vya Ikulu Jijijini Dar es Salaam, Katibu mkuu kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kuwa Rais Magufuli amaenza kazi kwa kumteua mwanasheria mkuu wa serikali ambaye ni George Mcheche Masaju aliyewahi kushikilia wadhifa huo, katika serikali ya awamu ya nne chini ya uongozi wa Rais mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete. Mwanasheria huyo mteule ameapishwa kuapishwa Ijumaa tarehe 6 Novemba 2015 majira ya saa nne asubuhi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali. Aidha Balozi sefue ameeleza kuwa Rais Magufuli ameitisha Bunge la 11 ambalo litafunguliwa rasmi tarehe 17/11/2015 nakuongeza kuwa huenda mpaka kufikia tarehe 19 mwezi huu Rais atakuwa amependekeza jina la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Serikali ya awamu ya tano na kusubiri ridhaa ya wabunge.

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anaweka historia ya kuwa ni mwanamke wa kwanza Tanzania kushika wadhifa wa kuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wachunguzi wa mambo wanasema, miaka ijayo, pengine Tanzania ikapata Rais wa kwanza mwanamke! Tanzania imewahi pia kuwa na Spika wa Bunge mwanamke Bi Anne Makinda. Hizi ni dalili za Serikali ya Tanzania katika kuwajengea wanawake uwezo katika masuala ya uongozi.

Sherehe za kuapishwa kwa Dr. John Pombe magufuli kuwa Rais wa awamu ya tano, zimepambwa kwa uwepo mkubwa wa Marais kutoka Afrika waliongozwa na Rais Robert Mugabe, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika. Rais Edgar Lungu kutoka Zambia, Rais Paul Kagame kutoka Rwanda; Rais Jacob Zuma kutoka Afrika ya Kusini, Rais Yower Kaguta Museven kutoka Uganda, Rais Uhuru Kenyatta kutoka Kenya pamoja na Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji. Tukio hili na kihistoria limehudhuriwa pia na Mawaziri wakuu pamoja na wawakilishi wa Jumuiya na Mashirika mbali mbali ya Kimataifa na Kikanda.

Watanzania wanaelekeza macho yao sasa katika uteuzi wa Waziri mkuu na Mawaziri watakaomsaidia Rais Magufuli kutekeleza dhamana yake ya kuwaongoza watanzania katika mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini, ukosefu wa ajira na hali ngumu ya uchumi, kila mtu akijitahidi kutekeleza wajibu wake. Wanasema, uteuzi wa Mawaziri uzingatie: uadilifu, ujuzi, uzalendo na kamwe usigubikwe na misingi ya urafiki, udini na ukabila, kama kweli Tanzania inataka kupeta katika mchakato wa maendeleo yanayojikita kwa watu kufanya kazi! Yaani hapa ni kazi tu! Hii ndiyo kauli mbiu ya Dr. John Pombe Magufuli, Rais wa awamu ya tano nchini Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.