2015-11-06 11:52:00

Hospitali ya Bambino Gesù ni kielelezo cha huduma ya upendo kwa watoto wagonjwa


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa mamlaka aliyokabidhiwa na Baba Mtakatifu Francisko ameteuwa wanachama wa Bodi ya ushauri kwa Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican pamoja na kupitisha Katiba mpya ya Mfuko wa Hospitali ya Bambino Gesù. Lengo ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ukweli, uwazi, mshikamano na tafiti, ili kuiwezesha Hospitali ya Bambino Gesù kutekeleza dhamana na wajibu wake hususan miongozi wa watoto wagonjwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Bodi ya ushauri itakuwa chini ya Rais Mariella Enoc, atakesaidiwa na: Pietro Brunetti, Ferruccio De Bortolo, Maria Bianca Farina, Caterina Maria Tarantola pamoja na Antonio Zanardi Landi. Mama Enoc,  kwa namna ya pekee anamshukuru Kardinali Pietro Parolin kwa kuwa karibu naye katika kipindi chote hiki cha mageuzi makubwa na matunda yake kuonekana kwa mara ya kwanza kwa mkutano wa Bodi ya washauri wa Hospitali ya Bambino Gesù pamoja na kupitishwa kwa Katiba mpya, dhamana iliyotekelezwa na Kardinali Pietro Parolin.

Mama Enoc anawashukuru wajumbe wote waliokubali kushiriki katika mchakato wa utekelezaji wa mageuzi yaliyoanzishwa, ili kuanza kuandika kurasa mpya kabisa, ikilinganishwa na siku za nyuma. Mfuko huu utakuwa na dhamana ya kukusanya fedha kwa ajili ya Hospitali ya Bambino Gesù, ili kusaidia tafiti mbali mbali za magonjwa ya watoto pamoja na kuendelea kufanya mageuzi kwa kutumia teknolojia mpya katika tiba ya magonjwa ya watoto.

Hiki ni kielelezo cha upendo na mshikamano wa kimataifa ili kuwahudumia watoto wagonjwa wanaoendelea kuteseka kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kardinali Parolin katika ujumbe aliowaandikia wajumbe hawa anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu pamoja na kuwashukuru kwa kazi kubwa wanayoendelea kuitekeleza kwa ajili ya nafuu na tiba kwa watoto wadogo. Huu ni utume unaojikita katika sadaka, huduma na majitoleo bila kuangalia masilahi ya mtu binafsi, kama kielelezo cha wafuasi wa Kristo na zaidi wakati huu wanapomsaidia Khalifa wa Mtakatifu kutekeleza dhamana na wajibu wake wa upendo kwa ndugu zake wagonjwa na maskini.

Ni huduma inayojikita katika kanuni maadili, taaluma na weledi, ili kuuwezesha Mfuko wa Hospitali ya Bambino Gesù kutekeleza dhamana hii nyeti. Kardinali Parolin anawatakia kheri na baraka tele katika awamu  hii mpya inayojipambanua katika ukweli na uwazi, ustawi na maendeleo ya Hospitali ya Bambino Gesù. Ni matumaini yake kwamba, wataonesha upendo ili kweli Hospitali hii iweze kuwa ni kielelezo makini cha upendo ambao Baba Mtakatifu Francisko pamoja na watangulizi wake walipenda kuutekeleza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto wagonjwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.