2015-11-06 15:05:00

Fedha na mali ya Kanisa inatumika kwa uangalifu mkubwa!


Msemaji mkuu wa Sekretarieti ya Uchumi mjini Vatican amekanusha madai yaliyochapishwa hivi karibuni kwenye Vitabu viwili ambavyo vinazungumzia kuhusu hali ya fedha na uchumi mjini Vatican;  kwamba, Sektretarieti ya uchumi ya Vatican ambayo kwa sasa inaongozwa na Kardinali George Pell imekuwa na matumizi makubwa katika kipindi cha mwaka 2014 ilipoundwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko. Matumizi ya fedha kiasi cha Euro 500, 000 yalikwisha tolewa maelezo, lakini kwa makusudi kabisa mwandishi wa vitabu viwili, ameshindwa kuonesha ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa na Sekretarieti ya uchumi mjini Vatican.

Itakumbukwa kwamba, vitabu hivi ni mkusanyiko wa nyaraka za siri zilizovujishwa kutoka Vatican na hivyo kusababisha kashfa na kwamba, wahusika kwa sasa wanashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama, ili waweze kushughulikiwa kisheria. Kitabu cha "Via Crucis" kimeandikwa na Gianluigi Nuzzi. ambaye anatumia nyaraka za siri kutoka Vatican ambazo tayari zimekwishafanyiwa kazi, kama alivyofafanua Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican na kwamba, mwandishi anataka kuchafua hali ya hewa mjini Vatican kwa ajili ya mafao yake binafsi.  

Hii ni taarifa ya fedha kati ya Mwezi Marchi hadi Desemba 2014. Fedha hii ilitumika kwa ajili ya kununulia vifaa vya ofisi, mishahara ya wafanyakazi, usafiri; ununuzi wa vifaa na mavazi ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Kikanisa cha Sekretarieti pamoja na nauli ya viongozi wakuu wa Sekretarieti. Kiasi hiki cha fedha kimetumika pia kwa ajili ya kulipia malazi kwa viongozi wakati walipokuwa nje ya eneo la kazi bila kusahau gharama ya ushauri kwa wataalam mbali mbali kuhusiana na masuala ya fedha na uchumi.

Taarifa kwa vyombo vya habari inakaza kusema, Sekretarieti ya uchumi imekuwa ikijitahidi kubana matumizi kwa kutumia fursa mbali mbali zinazojitokeza. Kanuni, sheria na taratibu za sasa ni kuhakikisha kwamba, matumizi yote ya fedha yanapitishwa kwanza kabla ya fedha kuanza kutolewa. Sekretarieti imepunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya fedha za Kanisa na kama inavyojionesha kwenye bajeti yake kwa mwaka 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.