2015-11-05 08:32:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 32 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, ninakuleteeni tafakari Neno la Mungu lililo taa na mwanga wa maisha yetu. Tayari tuko ukingoni mwa mwaka wa Kanisa, ni Dominika ya 32 ya mwaka B wa Kanisa. Mama Kanisa ametuwekea Neno likitualika kujitoa na kujiaminisha katika Bwana bila kujibakiza, tukiwa na matumaini na kwa namna hiyo tutajaliwa yale yote mema yatokayo kwa Mungu. Ujumbe huu tunaupata kwa mifano hai ya wajane wawili wanaokubali mpango wa Mungu na kutoa kile chote walichokuwanacho, kinyume na matajiri. Matokeo ya tendo lao jema wanakirimiwa baraka tele katika maisha yao.

Katika Somo la kwanza tunamwona Nabii Eliya akimkimbia mfalme Ahab ambaye alitaka kumwangamiza. Nabii anapokimbia anakutana na mama mjane ambaye yuko katika taabu ya njaa! Nabii akitambua taabu ya mama huyu lakini pia akiwa na tumaini katika Bwana, anamwomba maji na kipande cha mkate. Mama huyu alikuwa na unga kidogo kiasi cha kutosheleza siku moja kwa ajili yake na mwanaye, na baada ya hapo kadiri ya mjane huyo basi wangekufa! Lakini kwa sababu ya tumaini kuu na akisikiliza sala ya msisitizo ya Nabii Eliya anakubali kutoa kila kitu. Kwa ufadhili huu alioufanya kwa Nabii wa Mungu, mjane huyu anapata chakula cha kutosheleza maisha yake mpaka njaa itakapoisha katika nchi ile.

Mpendwa mwana wa Mungu, ukarimu na tumaini la mjane huyu ndio unaozaa matunda mema. Matunda haya ni baraka na amani itokayo kwa Mungu. Ni alama ya kwamba Mungu huwajali walio maskini ambao wanamkimbilia na kumtumaini daima katika maisha yao. Mungu huwajali wale wote ambao wanakubali kushirikisha vipaji vyao na kugawana mali zao na wengine walio wahitaji. Jaribu kuwa mkarimu kwa Mungu utaona matunda yake!

Ewe ndugu msikilizaji, bado tunaendelea na sehemu ya barua kwa Waebrania ambayo leo yatufundisha kwa msisitizo, tofauti iliyopo kati ya Kuhani mkuu wa kweli yaani Yesu Kristo na makuhani wengine. Yesu Kristu anatolea sadaka yake si katika madhabahu yaliyotengenezwa kwa mawe bali ukuhani wake ni wa madhabahu ya mbinguni ambayo hayakujengwa kwa mikono ya wanadamu. Kuhani Mkuu Yesu Kristo hutolea sadaka mara moja na hutosheleza maisha yote kwa kuondoa dhambi na kutakasa mioyo ya watu, tofauti na sadaka za makuhani wa Agano la Kale ambazo hazikumaliza shughuli ya kuwatakasa watu, kumbe iliwapasa kurudia kila mwaka! Basi mwaliko kwetu ni kumfuasa Bwana kwa kushiriki sadaka ya Misa kwa ajili ya wokovu wetu.

Katika Injili, Mtakatifu Marko akinukuu mafundisho ya Bwana anakazia kujitoa bila kujibakiza kama mama mjane aliyetoa sadaka senti mbili ambazo ilikuwa ndiyo hazina yake! Anatoa yote bila kuogopa kwa maana analo tumaini katika Bwana ambaye ni mgawaji wa mapaji yote. Mjane huyu ni kinyume na watu wengine ambao hutoa ziada na si mali hasa inayotoka katika mioyo yao! Mpendwa yafaa kujitazama moyoni wapi ulipo katika makundi haya mawili! Kama uko katika kundi la mjane basi unayo heri ya milele na uishikilie kwa furaha maana ni zawadi toka kwa Bwana.

Basi mpendwa ndugu unayetafakari nami, jaribu kujikuza katika sala ukiomba fadhila ya ukarimu katika maisha yako. Kula, ishi, cheka na zungumza na wengine kwa furaha daima.

Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.