2015-11-04 08:00:00

Watanzania dumisheni haki, amani na utulivu!


Mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Tanzania umetikisa msingi wa umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, kiasi cha kuacha kurasa chungu kwa baadhi ya wananchi katika medani za kisiasa na kidemokrasia. Viongozi wa dini wanaendelea kuwahimiza watanzania na wote wenye mapenzi mema kuonesha ukomavu wa kisiasa na kidemorasia kwa kuendelea kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa. Kamwe uchaguzi mkuu uliopita kisiwe ni kisingizio cha kuvuruga amani na utulivu nchini Tanzania.

Pale ambapo haki haikutendeka, sheria, taratibu na kanuni za nchi zifuatwe kikamilifu badala ya baadhi ya watu kujichukulia sheria mikononi mwao, kwani wanaweza kulitumbukiza taifa katika maafa makubwa, kama ambavyo mara nyingi inajitokeza kwa nchi nyingi za Kiafrika mara baada ya uchaguzi mkuu. Watanzania waoneshe umoja na ushirikiano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Padre John Maendeleo, Mkurugenzi wa Radio Maria Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, akiwa mjini Roma amepata nafasi ya kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani na utulivu nchini Tanzania mara baada ya uchaguzi mkuu. Ameshuhudia unyenyekevu, umoja na mshikamano wa watanzania. Anakaza kusema, nyingi za Kiafrika zinaendelea kuwa na vita, kinzani na migogoro mingi kutokana na baadhi ya watu kukumbatia udini, ukabila na umajimbo, sumu kali sana katika mafungamano, ustawi na maendeleo ya wengi.

Padre John Maendeleo anawataka watanzania kuendelea kushikamana katika umoja na upendo, huku wakiendelea kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya mafao ya watanzania wote. Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani umepita na washindi wametangazwa. Kuna kasoro ambazo zimejitokeza kwenye baadhi ya maeneo na mahali pengine matokeo ya uchaguzi kufutwa kabisa. Watanzania waoneshe ukomavu kwa kujikita katika sheria, amani na utulivu, ili haki iweze kutendeka. Haya ni mambo msingi kuendelezwa mara baada ya uchaguzi mkuu, vinginevyo, Tanzania ambayo kwa miaka mingi imekuwa ni kisiwa na cha amani, inaweza kujikuta amani inatoweka na badala yake maafa yanatawala!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.