2015-11-04 07:24:00

Mons. Angelo de Donatis kuwekwa wakfu, tarehe 9 Novemba 2015


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Jumatatu tarehe 9 Novemba, 2015 majira ya jioni anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumweka wakfu Askofu mteule Angelo de Donatis, aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Roma. Kabla ya uteuzi huu Askofu mteule De Donatis alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Marko Mwinjili iliyoko Campidoglio, Roma.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule De Donatis alizaliwa kunako mwaka 1954 huko Casarano, Lecce, Kusini mwa Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapadrishwa kunako mwaka 1980 na kunako mwaka 1983 akajiunga na Jimbo kuu la Roma. Wakati wa kipindi cha Kwaresima kunako mwaka 2014 aliongoza mafungo ya maisha ya kiroho kwa Baba Mtakatifu na wasaidizi wake wa karibu.

Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, ni makao makuu ya Jimbo kuu la Roma na limejengwa kwenye kilima cha Laterani. Kutokana na umuhimu wake katika kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa, Siku kuu ya kutabarukiwa kwa Kanisa hili inaadhimishwa ulimwenguni kote. Hiki ni kielelezo cha umoja wa Kanisa chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, aliyepewa dhamana ya kuchunga, kuongoza na kuwaimarisha ndugu zake katika imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.