2015-11-04 10:37:00

Dr. John Pombe Magufuli kuapishwa kuwa Rais wa awamu ya tano, 5 Novemba 2015


Dar Es Salaam kumekucha! Viongozi wakuu kutoka katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, EAC, Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika pamoja nan chi marafiki wa Tanzania wanatarajiwa kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais Dr. John Pombe Magufuli, Alhamisi, tarehe 5 Novemba 2015. Itakumbukwa kwamba, Rais mteule Magufuli alitangazwa kuwa mshindi wa Urais hapo tarehe 29 Oktoba na kukabidhiwa cheti cha ushindi hapo tarehe 30 Oktoba 2015.

Wakati huo huo, Zanzibar imeingia katika mgogoro wa kisiasa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, ZEC, Mheshimiwa Jecha S. Jecha, kutangaza kufutwa kwa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 kutokana na kile alichoeleza kuwa ‘haukuwa huru na wa haki’. Uamuzi huo wa Mheshimiwa Jecha unapingwa na CUF ambayo mgombea wake, Maalim Seif Sharif Hamad, aliitisha mkutano na waandishi wa habari hapo kabla na kuwaoneesha alichodai kuwa ni karatasi halisi za matokeo ya kura kutoka katika vituo vyote visiwani humo zikionyesha kuwa ameshinda kwa asilimia 52.87.

Kadhalika, waangalizi mbalimbali wa ndani na wa kimataifa wamepinga hatua ya kufutwa kwa uchaguzi huo, baadhi wakiwa ni Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Afrika Mashariki na pia balozi za mataifa ya Marekani, Uingereza na Ireland ya Kaskazini.

Katika mazingira kama haya kuna haja ya kukumbatia misingi ya haki, amani na utulivu kwa kufuata taratibu, sheria na kanuni za nchi, ili Tanzania isitumbukie kwenye maafa makubwa kwa misingi ya tofauti za kisiasa. Amani ni dhamana ya watanzania wote kuhakikisha kwamba, wanailinda na kuidumisha kamwe wasikubali kuitelekeza, kwani kuitafuta baadaye itakuwa ni taabu sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.