2015-11-03 07:09:00

Wawili watiwa mbaroni kwa kuvujisha nyaraka za siri Vatican!


Baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama mjini Vatican kuhusiana na uvujaji wa nyaraka za siri kutoka Vatican, tayari watu wawili wanashikiliwa na Polisi ya Vatican kwa tuhuma za kujihusisha na uvujishaji wa nyaraka za siri, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha maadili ya kazi. Hawa ni Monsinyo Lucio Angel Vallejo Balda na Francesca Chaouqui, ambao kwa siku za hivi karibuni walikuwa ni wajumbe wa Tume rejea iliyokuwa imepewa dhamana na Baba Mtakatifu Francisko marekebisho makubwa katika miundombinu ya Vatican kuhusiana na masuala ya kiuchumi na kiuongozi, COSEA.

Itakumbukwa kwamba, Tume hii iliundwa na Baba Mtakatifu Francisko Julai 2013 na kuvunjwa baada ya kuhitimisha kazi yake.  Watuhumiwa hawa wako mahabusu na tayari wameanza kuhojiwa na vyombo vya mahakama vya Vatican chini ya usimamizi wa Professa Gian Piero Milano, mhamasishaji wa amani na Roberto Zannotti msaidizi wake. Kuvujisha nyaraka za siri kutoka Vatican ni kosa la jinai linaloshughulikiwa kisheria.

Nyaraka hizi zimetolewa kwa mwandishi wa habari ambaye anajiandaa kuchapisha kitabu. Vatican inakaza kusema, kama ilivyokuwa wakati mwingine uliopita, hiki ni kielelezo cha uvovu wa nidhamu na imani ambayo Baba Mtakatifu Francisko anawakabidhi baadhi ya waamini. Suala la kitabu hiki linaendelea kushughuliwa na vyombo vya sheria, ili haki iweze kutendeka na adhabu kutolewa kwa wahusika ili iweze kuwa ni fundisho kwa wengine. Suala hili linaweza kuchukua sura ya kimataifa, kwani ni jambo ambalo linakosa ukweli na uwazi na matokeo yake linapania kuvuruga pamoja na kuwa na tafsiri potofu kinyume cha yale yaliyokusudiwa. Ikumbukwe kwamba, huu si mtindo sahihi wa kutaka kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na wajibu wake katika kuliongoza Kanisa la Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.