2015-11-03 14:45:00

Papa- Ibada ya kuwakumbuka Marehemu ni wito :kufanya upya uchaguzi wetu


Jumanne tarehe 3 Novemba 2015 majira ya saa tano katika Kanisa Kuu la  Mtakatifu Petro,  Baba Mtakatifu Francisko, aliongoza Ibada ya Misa kwa nia ya kuwakumbuka na kuwaombea Makardinali na Maaskofu wote waliofariki mwaka huu.  Katika kipindi hiki, Kanisa liliondokewa na  Makardinali 15 , Patriaki I na Maaskofu 99 kwa idadi ya jumla. Barani Afrika Kanisa limepoteza maaskofu 10 wakiwemo watatu kutoka Shirikisho la Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA.

Akitoa homilia kwa ajili ya Marehemu hao, Papa Francisco alisema leo hii tunawakumbuka na kuwaombea ndugu hawa ambao walilipenda Kanisa kama mchumba wao, na sasa tunamwomba  Mungu wa huruma , awapokee katika furaha kamili na umoja na Watakatifu. Papa aliendelea kuwakumbuka marehemu akisema kuwa ni wajibu kutoa shukrani kwa ukarimu wao wa kuitikia wito Mtakatifu, kama ilivyotajwa katika neno la Injili na hasa kwanza kabisa kwa ajili ya uongozi wao na huduma yao. Na kwamba katika wakati huo wa kutolea sala na maombi kwa ajili ya ujira wao walioahidiwa kama "watumishi wema na waminifu" kama ilivyoandikwa katika Injili (Mathayo, 25,14-30), pia sisi tulio bado hai tumeitwa kufanya upya uchaguzi wetu katika kulitumikia Kanisa. 

Papa alieleza na kusisitiza juu ya kutumikia na si kutumikiwa, akirejea  tukio la Yesu kuwaosha miguu wanafunzi wake . Amesema Yesu mwenyewe alionyesha wazi kwamba,  kuwa kiongozi  si kuwa myapala lakini ni kutumikia (Marko 10:45), na kwamba mtu hawezi kuwa mchungaji mwema kama hayuko tayari kutoa hata  uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Anayekubali kutumikia anakuwa mtu wa kutoa, si katika vitu tu lakini hata nafsi yake. Papa aliendelea katika macho ya kidunia mtu huyo huonekana kama mtu anayepoteza, lakini kwa undani wake, kwa  anayeyapoteza maisha kwa ajili ya upendo wake Kristo, huwa na nguvu za kukishinda kifo na kuupa ulimwengu uzima. Anayetumikia huokoa. Kinyume chake, asiyeishi kwa ajili ya kutumikia wengine huyo hajiwekei dhamana kwa maisha ya baadaye.

Papa Francisco aliendelea kuzungumzia upendo wa Mungu, kwamba "Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanae pekee ili ulimwengu uweze kukombolewa naye. Na viongozi wa Kanisa na waamini wakiongozwa na upendo huo hupata hamu ya kutenda kama alivyo fanya Bwana wao, kuyaokoa maisha ya wengine. Upendo wa Mungu usiokuwa na kipimo wala mwisho, upendo unaoendelea kuwepo hata miisho ya  dunia. Na kama inavyo dhihirishwa katika Mkate wa Ekaristi unaotolewa kwa ajili ya wokovu wetu , uliopatikana kutoka katika kifo na kutupatia maisha yaliyojazwa na matumaini.

Na kwamba wakati huo wa matoleo ya Misa kwa ajili ya Wapendwa Makardinali na Maaskofu,pia inakuwa ni wakati wa kujiombea hata sisi tulio bado hai, kuomba neema ya kuimarishwa, kama  Mtume Paulo anavyohimiza: kuyageuza mawazo yetu kwa mambo yaliyo ya juu na siyo kwa yaliyo ya chini (Colosai 3.2); kwa ajili ya upendo wa Mungu na jirani, badala ya  kujali tu mahitaji yetu.

Papa amesisitiza na kutoa mwaliko kwa watu wote,  kutojiwekea hazina hapa duniani lakini juu mbinguni. Asema huo ndiyo msingi wa kuyafuata maisha ya Pasaka ya Bwana, yaliyo leta ukombozi na kutuweka huru dhidi ya mashaka na wasiwasi unaoletwa  mambo ya  kidunia,  ambayo hupita na kuteketea kabisa ndani ya hewa nyembamba. Na kwamba maisha hayo hayadai zaidi , ila kwenda kwake tu,  ambako kuna maisha, wokovu, ufufuo na furaha. Huko ndiko tutakuwa watumishi wake kulingana na mapenzi yake, si kama watwana lakini kama wana wake wapendwa walioyatoa maisha yao kwa ajili ya wokovu wa dunia.  

Na siku ya Jumatatu jioni Papa Francisco alitembea eneo la makaburi lililoko chini ya  Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, ambako alitolewa sala zake binafsi kwa ajili ya Roho za marehemu watangulizi wake katika Kiti cha Askofu wa Rome . Imekuwa ni kama utamaduni wa Mapapa katika siku hii ya kuwakumbuka na kuwaombea marehemu, Papa huteremka chini katika eneo la Makaburi ya watangulizi wake kutolea sala zake binafsi, kuomba huruma ya Mungu . 








All the contents on this site are copyrighted ©.