2015-11-03 09:34:00

Maaskofu Tanzania wanakutana na wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani anawaalika watawa kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema, Kanisa linatambua na kuheshimu maisha na utume wa watawa duniani, lakini kwa namna ya pekee nchini Tanzania. 

Maaskofu pamoja na wakuu wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume nchini Tanzania, wanakutana tarehe 4 Novemba 2015, Jijini Dar es Salaam ili kusali, kutafakari na kushirikishana mang’amuzi ya maisha na utume wa watawa nchini Tanzania. Hili ni kundi ambalo limeendelea kuchangia karama za mashirika yao sanjari na kushuhudia sura ya Kristo Yesu katika ulimwengu mamboleo. Huu ni muda wa kusali na kutiana shime kwa kutambua umuhimu wa watawa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Baraza la Maaskofu Katoliki linapania kukuza na kudumisha umoja na ushirikiano, nyenzo muhimu katika kuihudumia Familia ya Mungu nchini Tanzania. Hii ni fursa ya kusikiliza machungu, furaha na matumaini waliyo nayo watawa nchini Tanzania. Maaskofu kwa upande wao, watawashirikisha pia yale walio nayo ili kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa na kwamba, watawa ni baraka kuu kwa Kanisa la Tanzania. Licha ya mchango mkubwa unaotolewa na watawa nchini Tanzania, Baraza la Maaskofu Katoliki linapenda pia kukazia umuhimu wa majiundo makini katika mashauri ya Kiinjili ili kuimarisha maisha ya kitawa kwa kumuiga Kristo Yesu aliyekuwa mtiifu, fukara na mseja.

Askofu Ngalalekumtwa  katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakaza kusema watawa wamekuwa mstari wa mbele katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania. Ni watu waliochangia utume huu kwa njia ya sala, maisha, sadaka pamoja na majitoleo yao. Hii ni zawadi kubwa kwa Mungu na Kanisa. Ni wadau wakuu katika mchakato wa Uinjilishaji hususan katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya jamii. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linamhudumia mtu: kiroho na kimwili, kwa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.