2015-10-31 11:11:00

Kila zama na kitabu chake!


Ifuatayo ni hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania katika hafla ya kuagana na watumishi wa Umma, Jijini Dar es Salaam.

Nakosa maneno ya kutosha ya kubeba na kuelezea furaha yangu ya kujumuika nanyi leo kwa wingi wenu kwenye hafla hii ya kuniaga. Mmenigusa sana kwa ishara hii ya upendo mliyoionyesha kwangu. Si jambo la kawaida kwa Rais kuagwa na watumishi wa umma, wala si jambo la lazima. Hii ni ishara kuwa tumeishi vizuri na tunaachana vizuri. Nawashukuru sana kwa zawadi mlizonipatia, maana pia mmenipatia katika kuzichagua zawadi zenyewe. Zitanifaa sana katika maisha ya ustaafu.

Nakushukuru sana Katibu Mkuu Kiongozi na viongozi wenzako kwa kuandaa hafla hii na kwa maneno yako ya kunikaribisha kuzungumza. Umeeleza kwa ufasaha yale mambo ambayo kwa pamoja tumeweza kuyafanikisha katika utumishi wa umma, na yale ambayo hatukuweza kuyakamilisha lakini tumeyafikisha mahala penye muelekeo wenye matumaini ya kukamilika siku zijazo. Nawashukuru sana watumishi wa umma kwa risala yenu nzuri. Nimeisikiliza kwa umakini mkubwa na nimeipokea kwa mikono miwili. Ndani ya risala yenu yako maombi, ushauri na mapendekezo. Napenda kuwahakikishia kuwa nimeyapokea na nitayajumuisha katika Taarifa yangu ya Makabidhiano (Hand Over Notes) nitakayomkabidhi Rais ajaye ili ayazingatie na kuyapatia majawabu.

Shukrani kwa Watumishi wa Umma

Mabibi na Mabwana;

Nitakuwa mchoyo wa shukrani nisipowashukuru na kuwapongeza sana watumishi wa umma kote nchini kwa kazi kubwa mliyoifanya katika kipindi cha miaka 10 ya awamu ya nne. Ni uungwana kukiri kuwa, mafanikio na sifa ninazozipata, zimechangiwa kwa kiasi kikubwa na jitihada zenu. Jukumu langu kama Rais, ilikuwa ni kutoa uongozi na maelekezo wa nini kifanyike. Ninyi kwa kiasi kikubwa ndio mlioshauri, mliotafsiri na mliotekeleza maagizo na maelekezo niliyowapatia ambayo imezaa matokeo tunayojivunia nayo. Nawashukuru na kuwapongeza sana kwa kujitoa kwenu na kutekeleza kwenu wajibu wenu kwangu kama kiongozi mkuu na wajibu wenu kwa taifa.

Umuhimu wa Utumishi wa Umma

Mabibi na Mabwana;Umuhimu wa Watumishi wa Umma katika nchi yetu ni jambo lisilohitaji mjadala, ingawa ni jambo linalopaswa kusemwa ili lieleweke vizuri. Kumekuwepo na uelewa finyu juu ya umuhimu wenu na mchango wenu mkubwa katika ujenzi wa taifa letu. Ipo haja ya kuendelea kuelimisha umma na wanasiasa kuwa ninyi ni chombo cha umma, kwa ajili ya umma na mnautumikia umma wote mkiongozwa na uweledi, uzalendo na viapo vyenu kwa taifa. Serikali za Vyama zinapita, ninyi mnaendelea kuwepo ndio maana masharti yenu ya ajira ni masharti ya kudumu na pensheni.

Mafanikio ya Kujivunia

Mabibi na Mabwana;

Katika miaka 10 iliyopita, ukiachilia mbali mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii, kumekuwepo na mafanikio makubwa ndani ya utumishi wa umma. Awamu ya nne imejenga juu ya msingi mzuri ulioachwa na awamu zilizotangulia na kuboresha zaidi maslahi na utendaji kazi wa utumishi wa umma. Mtakubaliana nami kuwa tumepiga hatua za kuridhisha katika kuongeza ufanisi serikalini kwa kuboresha mifumo ya utendaji na ufuatiliaji wa kazi za serikali, ushirikishwaji wa watumishi katika maamuzi na uendeshaji wa serikali na uendelezaji wa maslahi ya watumishi wa umma. Kwa upande wa uboreshaji wa mifumo ya kazi tumefanya yafuatayo:

a)Kuanzishwa kwa mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Mfumo huu wa usimamizi na ufuatiliaji umeongeza uwazi na ufanisi kwa kushirikisha wadau wote katika sekta husika;

b) Kuanzishwa kwa Serikali Mtandao (e-government) ambapo tumewezesha kuanzishwa kwa Mfumo wa Ajira kwa Njia ya Kielektroniki (e-Recruitment), mfumo shirikishi wa utoaji wa huduma za serikali kwa njia ya simu za mkononi; ukusanyaji wa maduhuli kwa njia ya mtandao; na tovuti ya wananchi kwa ajili ya kupokea maoni ya wananchi;

c) Kuanzishwa kwa Mfumo wa Taarifa Shirikishi za Kiutumishi na Mishahara mwaka 2012 ambao umewezesha ufanisi katika uhifadhi na uchakataji wa Taarifa za kiutumishi na mishahara ya Watumishi. Mfumo huu umetuwezesha pia kubaini Watumishi hewa.

d) Kupitia Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma Sura ya 105, tuliunda Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma, Baraza la Majadiliano ya Pamoja ya Kisekta (Sekta ya Utumishi Serikalini, Sekta ya Elimu, Sekta ya Afya na Sekta ya Serikali za Mitaa).Tulianzisha pia Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa lengo kutatua migogoro ya kazi.

Mafanikio haya katika uboreshaji wa mifumo ya kazi, umewezesha pia uboreshwaji wa maslahi ya watumishi wa umma. Katika eneo hili ningependa kutaja kwa uchache yafuatayo:

a) Kuundwa kwa Tume ya Kuboresha Maslahi ya Watumishi wa Umma mwaka 2006 ambayo mapendekezo yake yaliwezesha kuhuishwa kwa Sera ya Malipo ya Mishahara na Motisha katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2010, na kuundwa kwa Bodi ya Mishahara na Maslahi katika Utumishi wa Umma mwaka 2012.

b) Kupandishwa kwa kima cha chini cha mshahara mwaka hadi mwaka kutoka shilingi 65,000kwa mwezi mwaka 2005/2006 hadi shilingi 300,000 mwaka 2015/16 (ongezeko la mara 5). Wakati huo huo kushusha Kodi ya Mapato (PAYE) kutoka asilimia 18mwaka 2005/2006 hadi asilimia 11mwaka 2015/16.

c) Kutolewa kwa Waraka wa Watumishi wa Serikali Na. 3 wa mwaka 2011 unaowawezesha Watumishi wa umma kukopa fedha taslimu za kununulia samani, vyombo vya usafiri au matengenezo ya vyombo vya usafiri. Kutokana na ufinyu wa bajeti, Serikali pia imeweka utaratibu wa mabenki na taasisi za fedha kukopesha Watumishi wa umma.

d) Kuboresha mfumo wa Bima ya Afya kwa Watumishi wa Umma kwa kuondoa madaraja katika utoaji wa huduma. Aidha, tumepitia upya na kuboresha mafao ya kustaafu ya watumishi wa umma. Naipongeza sana Mamlaka ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa kazi nzuri waliyoifanya katika eneo hili. Nafahamu kuwa bado yapo masuala machache ambayo yako mezani kwa majadiliano.

Mabibi na Mabwana;

Ninachoweza kusema ni kuwa, jitihada hizi kwa pamoja zimefanya Utumishi wa Umma kuwa ni mahala pazuri pa kufanya kazi na kimbilio hata la wafanyakazi walioko katika sekta binafsi. Ni ukweli ulio wazi kuwa, watumishi wa umma wanaopokea kima cha chini cha mshahara wana nafuu kimaisha kuliko wale wa sekta nyingine. Natambua bado tunahitaji kuboresha zaidi katika eneo hili. Mimi binafsi, nimetumia madaraka yangu ya urais kuhakikisha kuwa nyongeza na nafuu inapatikana kila mwaka kwa watumishi wa ngazi za chini wa Serikali. Naamini Rais ajaye aye atafanya hivyo, muhimu tu mchague vizuri.

Pamoja na ukweli kuwa jitihada hizi hazijatatua changamoto zote zilizopo, kilicho wazi ni kuwa tumeweka msingi imara wa kuzipatia majawabu ya uhakika changamoto za utumishi wa umma. Ni bahati mbaya kwamba dhamira yetu njema imekuwa ikielemewa na uwezo mdogo wa mapato ya Serikali. Utatuzi wa changamoto nyingi unategemea sana upatikanaji wa fedha za kutosha jambo ambalo halina jawabu la mkato. Tunapaswa tuendelee kufanya kazi kwa bidii, kuongeza tija, ukusanyaji wa maduhuli ili hatimaye tujenge uwezo wa serikali kutoa maslahi mazuri zaidi kwa watumishi wa umma.

Mambo Mengine ya Kujivunia

Mabibi na Mabwana;

Mambo Mengine ninayojivunia ninapoagana nanyi ni kule kuwapa nafasi za uongozi wanawake na vijana; na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi. Tuliingiza katika Kipengele cha 12 (4) cha Kanuni za Utumishi wa Umma za 2013 kisemacho, “Inapotokea mwanamke na mwanaume wametimiza vigezo sawa kwa kulingana, basi kipaumbele atapewa mwanamke”. Kila zilipotokea fursa za uteuzi sikuacha kuwateua wanawake katika nafasi za juu zikiwemo za Makatibu Mkuu, Naibu Makatibu Mkuu na Wakuu wa Taasisi za Serikali. Tulifanya hivyo kwa nia njema ya kurekebisha kasoro za kihistoria zilizowanyima wanawake fursa za uongozi ndani ya Utumishi wa Umma.

Nimeteua pia vijana wengi katika utumishi wa umma kadiri fursa ya kufanya hivyo ilipojitokeza. Lengo kubwa ilikuwa ni kuandaa na kuwalea vijana walioonyesha ari kuwa viongozi wa baadaye. Utumishi wa Umma lazima utambue vipaji mbalimbali na kuviendeleza na si kuvizima. Nimefanya hivyo pia kwa kuteua vijana kutoka sekta binafsi na kuwaingiza serikalini. Lengo langu ni kuleta serikalini changamoto mpya na mitazamo mipya ya utendaji kazi.

Mabibi na Mabwana;

Tulipo sasa na huko tuendako, tunapaswa kujenga uelewa wa kufaya kazi kwa ushirikano na sekta binafsi ambayo ni muhimili muhimu wa ujenzi wa nchi ya uchumi wa kati. Ndio sababu, nimejitahidi kuileta sekta binafsi karibu na kuwashirikisha na hivyo kuwafanya kuwa sehemu ya suluhisho badala ya wao kuwa sehemu ya tatizo. Tumewashirikisha katika uundaji wa maabara za BRN na tumefanya hivyo pia kupitia Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na kwa kuweka Sheria ya Ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (PPP). Sasa tunawashirikisha katika mapambano dhidi ya rushwa ambako sasa nao watasaini Hati za Uadilifu kama zile zitakazosainiwana viongozi wa umma na watumishi wa umma. Haya ni mambo ambayo nitafurahi kuona mkiyaendeleza.

Changamoto Mpya kwa Sekta ya Umma

Mabibi na Mabwana;

Utumishi wa Umma wa leo unapita katika kipindi chenye changamoto tofauti na huko tulikotoka. Mabadiliko katika mazingira ya kidunia, kisiasa na rika/demografia (demography) yanaathiri sana utamaduni na utendaji kazi katika utumishi wa umma. Wadau wa serikali wameongezeka na madai yao yamepanuka sawia. Kumekuwepo na mahitaji makubwa ya ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika maamuzi ya serikali, mapato na matumizi ya serikali na ushirikishwaji wa wananchi na sekta binafsi katika maamuzi na shughuli za serikali.

Hamna budi kujitazama upya na kuchukua hatua za kufanya maboresho na mageuzi kuendana na mazingira mapya. Ukiritimba usio na lazima, usiri usio na lazima na uhafidhina katika uendeshaji wa mambo hauna nafasi tena sasa na huko tuendako. CAG ametusaidia sana kuona mapungufu yetu. Nawapongeza kwa kuzifanyia kazi Taarifa zake kiasi cha yeye kukiri hivyo katika Taarifa ya CAG ya Ukaguzi ya mwaka ulioishia 30 Juni, 2014. Tumejitahidi kuondokana na hati chafu, sasa ongezeni juhudi kuondokana na hati zenye mashaka.

Mabibi na Mabwana;

Mnapaswa pia kuangalia namna mpya ya kuboresha mfumo wa mawasiliano wa serikali na umma. Awamu ya nne tumefanya mambo mengi makubwa lakini tumekuwa wazito katika kuyaelezea kwa kile tulichojizoesha kuwa ‘Chema chajiuza, kibaya chajitembeza’.Nawakumbusha kwamba zama hizo zimepita na hazitarudi tena. Kufanya mambo mazuri ni jambo moja, na kujulikana kwa mambo hayo mazuri ni jambo lingine, ambalo ndio muhimu zaidi. Hili ni jambo la kulifanyia kazi huko tuendako.

Wosia

Mabibi na Mabwana;

Nimesema mengi, lakini ningependa nimalizie kwa kuwakumbusha machache ambayo naona yana umuhimu wa kipekee kwa ustawi na uhai wa utumishi wa umma. Kwanza,nawaomba sana muheshimu viapo vyenu. Pili,zingatieni miiko na maadili ya utumishi wa umma ambayo ndio msingi na uhai wa utumishi wa umma. Hakuna serikali duniani isiyo na miiko au usiri wa masuala nyeti ya uendeshaji wa serikali. Uvujaji wa siri ni kielelezo kikubwa cha kuporomoka kwa maadili ya utumishi wa umma popote duniani. Mkifika hapo, maana yenyewe ya kuwa na serikali inakuwa ni kama haipo. Tatu, mtii sheria, kanuni na taratibu za utumishi wenu ili kuleta ufanisi na kuondoa migogoro na manung’uniko yasiyokuwa ya lazima.

Hitimisho

Mabibi na Mabwana;

Namalizia kwa kuwashukuru tena kwa hafla hii mliyoniandalia na zawadi mlizonipatia. Kwa nama ya kipekee, Nawashukuru Makatibu Wakuu Viongozi niliofanya nao kazi Mheshimiwa Balozi Marten Lumbanga, Mheshimiwa Philemon Luhanjo na Mheshimiwa Balozi Ombeni Sefue. Nawashukuru pia Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya, Makamishna, Mabalozi, Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Serikali na watumishi wote wa umma kwa mchango wenu mkubwa ulioniwezesha kutimiza wajibu wangu kwa watanzania kwa mafanikio makubwa.

Nafurahi kuwa, niliupokea utumishi wa umma kutoka kwa Rais wa awamu ya tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa ukiwa imara na katika hali nzuri. Nafarijika kwamba nitamkabidhi Rais ajaye utumishi wa umma ulio katika hali nzuri zaidi ya kuweza kumsaidia kutekeleza malengo yake na Ilani ya uchaguzi ya Chama chake. Nitapenda sana awe mwana CCM maana naamini mnamjua na hampatapa taabu ya kuendana naye na kutekeleza Ilani ya CCM ambayo ndio iliyo bora katika uchaguzi mkuu huu. Ninachowaomba, mpeni Rais mpya ushirikiano wenu kama au hata zaidi ya ule mlionipatia mimi. Muwe tayari kumsoma na kumuelewa matakwa yake, aina yake ya ufanyaji kazi na kasi yake. Msije mkasema, ‘Rais Kikwete alikuwa hafanyi hivi”. Kumbukeni ule msemo wa Mzee wetu Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa ‘Kila Zama na Kitabu Chake’. Nawatakia kila la kheri katika utumishi wenu. Nawaaga rasmi, kwaherini!

Mungu Ibariki Afrika,

Mungu Ibariki Tanzania.

Asanteni kwa kunisikiliza!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.