2015-10-31 15:11:00

Kazi yako ndilo jina lako! Hapa kazi tu Baba! Wavivu watafute mahali pengine!


Kuna lugha ya kudharau, kutia kichefuchefu! ya kusanifu, ya kukebehi, ya kukejeli na ya kutania wengine kwa lengo la kudhalilisha au kuleta maudhi pamoja na kutibua nyongo za watu! Wakati mwingine lugha hiyo hutumika ili kusifu. Kwa mfano, mtu aliye mahili kwa jambo fulani anaitwa: Mshenzi wa mbio ndefu, Mchawi wa mpira, Gwiji wa shairi” Nguli, Mbaya wa muziki, Tingatinga, Mwamba wa kutunga mashairi, nk. Lakini lugha hiyohiyo inaweza kuzua kizaazaa kumwita mmoja mchawi, mshenzi, tingatinga, mbaya, nk.

Mwanzoni mwa Kanisa Wafuasi wa Yesu walipachikwa majina kama hayo ya kebehi na kejeli. Waliwahi kuitwa Wagalilea, maana yake watu wa migomo na upinzani. Waliitwa pia Wanazareti yaani wanyamugi! Watu wa kuja! Watu kutoka porini nyumbani kwa Yesu, “Vyasaka”; . Halafu wakaitwa Wakristo jina lililotumika kwa mara ya kwanza kule Antiokia kuwaita wafuasi wa Yesu. Nao wakajisikia vizuri kwani Kristo maana yake mpakwa. Lakini kwa bahati mbaya mpakwa huyu aliishia pabaya kwani alikataliwa, alipigwa vibaya na kuuawa kwa kusulibiwa Msalabani kama jambazi. Hadi leo Wakristo tunaendelea kuitwa majina mengi ya kashfa kama vile, “Wala nguruwe, Kafiri, Wasekulolu, Wala vibudu, Warumi, nk.”

Leo tumesikia jina jingine “Watakatifu au Wenyeheri.” Kwa vigezo vya kibinadamu Mwenyeheri ni yule aliyefanikiwa, aliyeshinda mitihani, uchaguzi mkuu, aliye na mali, tajiri. Huyo tunamsema  kuwa ni mwenyeheri, ameukata, amefanikiwa, mtakatifu. Kwa upande mmoja, watakatifu au wenyeheri tunaowashangilia leo ni marehemu waliotutangulia, kwa vigezo vya fadhila waliyokuwa nayo walipokuwa hai na kutokana na miujiza waliyofanya. Kwa upande mwingine, Mungu anatufagilia sisi tulio hai kuwa watakatifu anaposema: “Watakatifu waliopo duniani ndio walio bora, hao ndio niliopendezwa nao.” (Zab. 16:3) Kwa hiyo hata sisi leo tunajitangazia ushindi, kwani sisi tunaweza bado kutenda matendo ya kumpendeza Mungu. Hata hivyo sisi sote marehemu na wazima, hatustahili kuitwa watakatifu kutokana na wimbo wa “Utukufu kwa Mungu juu” usemao: “Kwa kuwa ndiwe uliye peke yako Mtakatifu, peke yako Bwana, peke yako mkuu, Yesu Kristu.” Kulikoni tuitwe Watakatifu?

Ukweli ni kwamba, watoto au wafuasi tu wa aliye Mtakatifu ndiyo wanaweza kustahili kuitwa Watakatifu. Ndiyo maana Paulo mtume anawaita wafuasi na washiriki wa mateso ya Yesu kuwa ni watakatifu kila anapowaandikia barua ya kichungaji: “Kwa watakatifu wote walioko Roma, Korinto, Filipo, Kolosai, Efeso, nk.  Utakatifu na Wenyeheri wa Yesu unao vigezo vyake visivyofuata katiba ya binadamu. Katiba ya Yesu ina vipengele nane tu. Juu ya vipengee hivyo Origene alisema, kuwa “Heri nane” ni picha au ikona ya kiroho ya Yesu aliye Peke yake mtakatifu. Kwa hiyo mfuasi wa Yesu hana budi kuakisi sura na picha yake. Hebu tuiangalie katiba hiyo na tuone pia jinsi ilivyochakachuliwa na binadamu.

Mosi, “Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Kipengee hiki cha katiba kimehakachuliwa kwa maelezo, kwamba mwenye heri ni tajiri lakini anagawa kwa maskini. Mbaya ni tajiri asiyegawa na anatumia mali kibinafsi. Kwa hiyo ukitaka kuwa mwenyeheri budi uwe maskini. Kumbe Mungu ametuumba kwa upendo na ametuwekea tayari mali ulimwenguni ili tusiteseke. Mali hiyo yatakiwa igawanywe kadiri anavyotaka Mungu ili kila mmoja awe na furaha. Kwa hiyo maskini wa roho ni nguvu ya kimungu iliyo ndani mwetu inayotusukuma kutokutawala wala kutawaliwa na mali, na akili na maweza yetu, na kwamba vitu vyote ni vya Mungu. Tuvitumie kwa upendo. Hapo tulichokitoa kinageuka kuwa upendo ambao ni Mungu mwenyewe.

Pili, “Heri wenye huzuni, maana hao watafarijika.” Kipengee hiki nacho kimechakachuliwa hasa na wakereketwa wa dini, wanaoongeza chumvi katika huzuni na uchungu hadi kufikia hatua ya kujitesa, kujisulubu na kujipatia maumivu yakidhaniwa kuwa ni alama ya wongofu na utakatifu kwa ajili ya Mungu. Kumbe huzuni siyo kuteseka. Neno la kigiriki penthountes maana yake kuishi kwa huruma, ni kuwajibika kujenga ulimwengu mpya kadiri ya mapenzi ya Mungu. Mfuasi wa Kristo hawezi kutulia asipate huzuni anapoona ulimwengu wa kinafiki, wa uwongo, wa kugandamizana na usio na thamani za kienjili. Mwenye heri anahuzunika kwa vile anataka kujenga ulimwengu mpya kadiri ya huruma ya Mungu. Kwa wale wanaoona uchungu huo wameahidiwa kutulizwa kwa sababu Mungu atakuwa pamoja nao katika harakati zao za kujenga ulimwengu mpya wa Mungu.

Tatu, “Heri wenye upole, maana hao watairithi nchi.” Kwa lugha ya kawaida mpole ni yule asiyejibu mapigo anapopigwa. Aliyetulia na hashtuki anapochokozwa au kuumizwa. Tafsiri hiyo imechakachuliwa. Mzaburi anatuambia: “Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya, usiwahusudu wafanyao ubatili.” (Zab. 37:1). Heri hiyo ni ya matumaini. Tunamwiga Kristu aliyesema: “Jifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.” Haina maana kwamba alipodhulumiwa alikaa kimya kama bwege, la hasha, bali aliishi madhulumu yaliyomfanya kuwa mpole. Yesu alijibu uovu kwa upendo na siyo kwa ovu.

Nne, “Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa.” Kula na kunywa ni haki ya msingi kwa maisha. Haki na upndo wa kugawana mali ni fadhila za Mungu yake anayetaka ulimwengu mpya wa upendo. Kwa hiyo Heri wanaowajibika yaani wanaohaha, wanaochakalika ili kila mmoja apate mahitaji ya lazima, ili kuujenga ulimwengu wa Mungu kama mwenye njaa na kiu anavyohaha kutafuta chakula kula na kinywaji.

Tano “Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema.” Maana inayoonekana mara moja na wachakachuaji ni kwamba rehema kwao ni kusamehe makosa yanayostahili adhabu. Kumbe tunaambiwa kuwa Mungu ana rehemu lakini pia anaadhibu uovu na udhulumu. Upendo ni haki ya Mungu, na kuonea huruma hakuwezi kuuzuia upendo wake. Kuwa na huruma kunamaanisha hali tatu: Kwanza, kuelewa mahitaji ya wengine kama alivyofanya Msamaria aliyekuwa anaenda Yerusalemu. Pili, kuonea huruma, yaani kulia na wanaolia. Tatu, kuingilia kati yaani kufanya kitu. Kwa hiyo mwenye huruma, au rehema ni yule mwenye roho inayoona na kuingilia kati kusaidia maskini Mtu huyo ana fikra moja na Mungu aliye na huruma na upendo.

Sita, “Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu.” Moyo ni makao ya maamuzi safi bila vionjo. Kwenye moyo kuna udhaifu mwingi wa kutamani mali, utajiri, ukuu. Kwenye moyo kuna miungu ya uwongo inayovuruga mawazo na fikra safi za kimungu. Kitu safi ni chenyewe kinavyoitwa na kinavyotakiwa kuwa. Kwa hiyo kuwa na moyo safi, maana yake kufanya uchaguzi unaoongozwa na Mungu aliye safi.

Saba, “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Wapatanishi ni wale wanaowajibika katika kujenga amani ya ulimwengu. Wanaowajibika ili ulimwengu usiwe na ujinga, usione njaa na kiu. Wanaojenga amani hiyo, wanafanana na Mungu kweli.

Nane, “Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni wao.” Ulimwengu una katiba yake yenye vigezo vyake vya mafanikio na unainadi kwa nguvu sana katiba yake. Yesu naye anayo Katiba yake yenye vipengee nane vya mafanikio. Katiba hizi mbili zipo katika mvutano na mapigano ya kudumu. Kwa vyovyote mwisho mwishoni, mmoja atatangazwa tu mwenye heri kwa vigezo vya katiba ya chama tawala, yaani Kristo. Kwa hiyo Hapa ni kazi tu! Utafanikiwa kuishi maisha ya heri ya Kristo kwa kumwiga Bikira Maria, aliyeambiwa na shangazi yake Elizabeth. “Una heri wewe, kwa sababu ulisadiki ukayakabidhi maisha yako yote kwa Mungu. Heri kwa Sikukuu ya Watakatifu wote.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.