2015-10-30 08:37:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe ya Watakatifu Wote!


Tunakuletea habari njema ya furaha tunapotafakari pamoja Neno la Mungu katika sherehe ya Watakatifu wote. Mama Kanisa akitaka kuhitimisha mwaka wa Kanisa kwa furaha anaona ni vema awaoneshe watoto wake lengo la maisha ya kikristu yaani ni kuelekea maisha ya utakatifu, maisha ya milele mbinguni. Kumbe Mama Kanisa amependa kila tarehe Mosi Novemba ya kila mwaka, sherehe hii iadhimishwe katika Kanisa zima la kiulimwengu. Adhimisho hili ni mwaliko kwetu kuchuchumalia maisha yanayotimiza mapenzi ya Mungu, maisha ya ufufuko ambayo Mtume Paulo anatuambia daima akisema basi mkishafufuliwa mkayatazame yaliyo ya juu!

Mpendwa, yafaa kutambua watakatifu ni akina nani? Watakatifu ni wale wanaokaa na Mungu katika kiti chake cha enzi kadiri tusomavyo katika kitabu cha Ufunuo. Ni marafiki wa kweli au tunaweza kusema ni marafiki wa dhati au wa kina. Ni wale ambao Injili ilikuwa chakula chao cha kila siku walipokuwa duniani na walijikabidhi katika mikono ya Mungu na kuwa mali yake. Ni wale walioishi heri nane mafundisho ya Kristu aliyoyatoa pale mlimani. Ni wale ambao walitunza neema ya UTAKASO waliyoipokea wakati wa Ubatizo. Ni wale ambao walimpenda Mungu kwa moyo wao wote, kwa akili yao yote na kwa nguvu zao zote na kisha wakampenda jirani aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni wale ambao katika ubinadamu wao walikubali mateso wakitambua na kujua siri ya furaha watakayoipata milele. Sasa wanafurahia matunda ya msalaba wa Kristu. Kwa kifupi ni wale walioshika vema amri kuu ya mapendo.

Ili basi nasi tuweze kufikia hali hiyo iliyo heri na furaha upeo, somo la kwanza linaweka  mwaliko kwa watu wote kuwa, ili mmoja aweze kupokea heri za milele yaani utakatifu, ni lazima kufua mavazi katika Damu ya Mwanakondoo. Ni lazima kukinywea kikombe kimoja cha Damu Takatifu iliyo thamani ya wokovu kwa wote. Ndiyo kusema ni kuishi kwa kutimiza mapenzi ya Mungu. Kwa kufua mavazi katika Damu ya Mwanakondoo kunamwondoa mtu katika dhiki ya dhambi na dhiki ya upungufu wa upendo mkamilifu. Mmoja ananyakuliwa toka taabu ya ulimwengu geugeu na kuvikwa mavazi meupe ndiyo utakaso mkamilifu unaowezesha kuimba baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina. Huu ni wimbo wa sifa kwa Mungu ambao unaweza kuimbwa na walio wake, ndiyo watakatifu.

Katika Injili ya Mathayo tunapata mafundisho ya Yesu mlimani yaani Heri Nane. Bwana anaonesha njia ya kufikia utakatifu, njia ya kuishi mapenzi ya Mungu. Anaainisha namna ya kufika mbinguni, akisema, wanaheri wale walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao. Wanaheri wenye upole maana watairithi nchi. Anazidi kukazia utakaso wa roho akisema heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu. Hizi ni baadhi ya heri nane za mlimani njia kamilifu ya kufikia utakatifu.

Kwa kuzitafakari heri nane tunaweza kusema mambo makuu mawili ni lazima katika kufikia utakatifu. Jambo la kwanza ni kujitenga na chachu ya ulimwengu. Kumbuka Bwana anasali na kusema tuko ulimwenguni lakini sisi si wa ulimwengu. Hii yamaanisha kujitenga na kile kinachopingana na Injili ya Bwana, na hivi kuwa maskini wa roho. Kumbe mkristu anapaswa ajisikie daima kinyume na mawimbi ya ulimwengu yanayopingana na Injili. Jambo la pili ni lile la kupokea kikombe cha mateso daima na kulitangaza jina la Bwana. Mateso haya hugeuka na kuwa furaha katika maisha ya mkristu sasa anapoishi na baadaye.

Mtakatifu lazima aoneshe sura ya Kristu mteswa na mwenye furaha kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Mtakatifu ni lazima amwilishe Heri Nane katika maisha yake na hivi zingae daima na kuwa kielelezo cha maisha ya upendo kwa Mungu na kwa watu. Mpendwa hiyo ndiyo habari ya upendo mkamilifu utokao kwa Mungu kwa ajili ya watu wote, na sasa unaalikwa kushiriki zawadi hii ya upendo bila kuchelewa tunapowashangilia watakatifu wa Mbinguni.

Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.