2015-10-30 13:59:00

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa, tarehe 30 Oktoba 2015 anasema, Padre mwema ni mtu anayeguswa na shida pamoja na mahangaiko ya watu wake, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza hata kidogo. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, kamwe hachoki kusamehe na kusahau. Mungu anasamehe kama Baba mwema na wala si kama hakimu mahakamani. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu ana huruma kwa kila binadamu na kwa wanadamu wote katika ujumla wao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika sehemu ya Injili ya Baba mwenye huruma, waamini wote wanajitambua kwamba, ni wakosefu na wanahitaji huruma na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayejishusha kabisa ili kumsaidia na kumhudumia mwanadamu, kutoka katika undani wa moyo wake. Ni kutokana na huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka, Mwenyezi Mungu alimtumwa Mwanaye wa pekee, Yesu Kristo ili aje kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hatimaye, kumshirikisha maisha ya uzima wa milele.

Yesu aliwaponya wagonjwa kama kielelezo cha ushuhuda wa Mungu anayeponya, anayeokoa na kuwalinda watu wake kama inavyojidhihirisha pia kwa  mfano wa Kondoo na shilingi iliyopotea. Mwenyezi Mungu anasamehe na kuponya kutoka katika undani wa moyo wake! Hii ndiyo dhamana inayopaswa kutekelezwa na Mapadre kwa kuguswa na mahangiko ya watu wao, tayari kujisadaka ili kuwasaidia kwa hali na mali, kwa kumuiga Yesu Kristo, kuhani mkuu. Padre mwema na mtakatifu aguswe na kushiriki katika mateso, furaha na mahangaiko ya watu wake.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, amempongeza Kardinali Javier Lozano Barragàn ambaye, ameadhimisha kumbu kumbu ya miaka 60 tangu alipopewa Daraja takatifu la Upadre. Akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa katika Baraza la Kipapa  la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya. Miaka 60 ya huduma iliyotukuka ndiyo zawadi kubwa ambayo Kardinali Barragàn amezawadiwa na Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.