2015-10-30 14:56:00

Kumbu kumbu ya Marehemu wote!


Kila mwaka ifikapo tarehe 2 Novemba, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Marehemu wote kwa kuwakumbuka na kuwaombea  waamini wote waliolala katika usingizi wa amani wakiwa na tumaini la ufufuko, ili waweze kusafishwa dhambi zao tayari kushiriki utukufu wa Baba yao wa mbinguni. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe Mosi Novemba, Siku kuu ya Watakatifu wote, majira ya jioni atawaongoza waamini wa Jimbo kuu la Roma pamoja na watu wenye mapenzi mema katika Ibada ya Misa Takatifu, atasali na kuwaombea Marehemu wote pamoja na kubariki makaburi yaliyoko kwenye eneo la Verano, Jimbo kuu la Roma. Ibada ya Misa takatifu inatarajiwa kuanza majira ya saa 10: 00 kwa kuwashirikisha viongozi mbali mbali wa Jimbo kuu la Roma. Ibada kama hii zitaadhimishwa pia kwenye makaburi mengine ya Jimbo kuu la Roma kwa kuongozwa na Maaskofu wasaidizi pamoja na Maparoko walioko kwenye maeneo haya.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 2 Novemba 2015, majira ya jioni anatarajiwa kutembelea na kusali kwenye Makaburi ya viongozi wa Kanisa waliozikwa ndani ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, tarehe  Mosi, Novemba, Siku kuu ya Watakatifu wote ilianzishwa na Mtumishi wa Mungu Guglielmo Giaguinta, pole pole ikaenea Jimbo kuu la Roma na hatimaye kuanza kuadhimishwa na Kanisa zima, ni mwaliko kwa waamini kuchuchumilia ukamilifu na utakatifu wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.