2015-10-30 14:42:00

CELAM iendelee kuwa ni chombo cha wongofu wa kichungaji na kimissionari


Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuungana na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM wakati huu linapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, chombo makini cha huduma ya Kanisa la Mungu Amerika ya Kusini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, CELAM itaendelea kujikita katika mchakato wa wongofu wa kichungaji na kimissionari, kwa kuwashirikisha waamini wengi zaidi katika azma ya Uinjilishaji mpya katika medani mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kukazia umuhimu wa Jumuiya za Kikristo kuwa kweli ni shule ya umoja unaojikita katika udugu unaotambua asili yao kuwa ni Baba mmoja, ili kuendelea kulipyaisha Kanisa huko Amerika ya Kusini; kwa kuguswa na mahangaiko pamoja na shida zao, ili kutoa majibu muafaka kwa changamoto wanazokabiliana nazo kwa sasa kwa kujikita katika misingi ya usawa, haki na amani.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, kitakuwa ni kipindi cha neema, mwaliko kwa CELAM kuhakikisha kwamba, inatoa huduma makini katika kuhamasisha, kushirikisha na kuadhimisha tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anapenda kuhitimisha ujumbe wake kwa kuwapatia baraka zake za kitume waamini wote wa Amerika ya Kusini na Caraibi, kwa kuwafunika na joho la Bikira Maria, Mama yetu wa Guadalupe pamoja na Kristo Yesu ili waweze kuhamasisha ari na moyo wa kimissionari ili Kanisa liweze kupata watakatifu wapya, wajenzi wa misingi ya haki na amani katika mataifa yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.