2015-10-29 08:34:00

Padre Giacomo Morandi ateuliwa kuwa Katibu mkuu msaidizi: Mafundisho tanzu


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Giacomo Morandi, kutoka Jimbo kuu la Modena-Nonantola, Italia kuwa katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la mafundisho tanzu ya Kanisa. Padre Morandi alizaliwa tarehe 24 Agosti 1965 baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa kunako tarehe 11 Aprili 1990. Baadaye akajiendeleza katika masomo ya juu na kujipatia Shahada ya kwanza katika Sayansi ya Maandiko Matakatifu kwenye Taasisi ya Biblia, Chuo Kikuu cha Gregorian kunako mwaka 1992.

Akajiendeleza zaidi na hatimaye kujipatia shahada ya uzamili na uzamivu katika taalimungu ya Uinjilishaji kwenye Chuo kikuu cha Gregorian kunako mwaka 2008. Tangu wakati huo, amekuwa akitekeleza dhamana na utume wake wa Kipadre katika masuala ya katekesi, Uinjilishaji, utamadunisho na uongozi Jimbo kuu la Modena-Nonantola. Ni Jaalimu wa sayansi ya Maandiko Matakatifu na Mafundisho ya Mababa wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.