2015-10-29 15:43:00

Mfuko wa Elimu ya Kikristo waanzishwa mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kuanzishwa kwa Mfuko wa Elimu ya Kikristo kama sehemu ya kumbu kumbu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha tamko kuhusu umuhimu wa Elimu ya Kikristo, Gravissimum educationis kunako tarehe 28 Oktoba 1965 unayokazia pamoja na mambo mengine ni: umuhimu wa elimu katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, ili waamini waweze kufaidika na urithi wa kitamaduni na maisha ya kiroho. Pili ni kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya kijamii. Kanisa linatambua kwamba, elimu ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kwamba, kila binadamu ana haki ya kupata elimu bora inayoambata pia elimu ya Kikristo.

Baba Mtakatifu Francisko analipongeza kwa namna ya pekee Baraza la Kipapa la elimu Katoliki kwa kuanzisha Mfuko wa Elimu ya Kikristo ili kusaidia mchakato wa waamini kupata elimu, ujuzi na maarifa ya kisayansi tayari kuendeleza Elimu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu ameamua pia kwamba, Makao makuu ya Mfuko wa Elimu Katoliki yawe katika mazingira ya mji wa Vatican. Mfuko huu utaongozwa na kusimamiwa na sheria, kanuni na taratibu zote za mji wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.