2015-10-29 08:57:00

Kardinali Scola: Papa Francisko kutembelea Jimbo kuu la Milano, 7 Mei 2016


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Jimbo kuu la Milano, Italia, tarehe 7 Mei 2016, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, sanjari na kuwasaidia kufahamu na kumwilisha huruma ya Mungu katika safari ya maisha yao ya kiroho. Ni maneno ya Kardinali Angelo Scola, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano wakati akiwatangazia waamini wa Jimbo lake, kuhusu tukio kubwa la kihistoria katika maisha na utume wa Kanisa.

Familia ya Mungu Jimbo kuu la Milano, inapenda kumshukuru Baba Mtakatifu kwa kuamua kuwatembelea ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo, tayari kumwilisha huruma ya Mungu kati ya watu wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku. Ni matumaini ya Jimbo kuu la Milano kwamba, hii itakuwa ni Habari Njema kwa wananchi wa Mkoa wote wa Lombardia.

Hii ni hija inayofanyika wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, mwaliko kwa Mama Kanisa kufanya upembuzi wa kina kuhusu ukweli katika upendo unaovyomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa nyakati hizi. Ni huruma na upendo wa Mungu uliokaziwa kwa namna ya pekee na Mababa wa Sinodi ya familia iliyohitimishwa hivi karibuni mjini Vatican.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko Jimbo kuu la Milano ni ya kichungaji, ili kuwahamasisha waamini kujifunga kibwebwe tayari kutoka kimasomaso kumtangaza na kumshuhudia Kristo katika uhalisia wa maisha yao, huku wakiendelea kuambata Injili ya familia, inayokabiliwa na changamoto nyingi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Waamini wanahamasishwa kujikita katika ari na moyo wa kimissionari, tayari kutweka hadi kilindini ili kushiriki katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Ni mwaliko wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wao pia waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, tangu wakati huu wanaalikwa kujiandaa kwa njia ya sala, ili kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko atakapowatembelea Jimboni humo hapo tarehe 7 Mei 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.