2015-10-29 16:37:00

Dr. John Pombe Magufuli wa CCM ndiye Rais mteule wa Tanzania!


Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania, NEC, Jaji mstaafu Damiani Lubuva, Alhamisi tarehe 29 Oktoba 2015 amemtangaza Dr. John Pombe Magufuli kuwa ni mshindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Tanzania, hapo tarehe 25 Oktoba 2015.  Rais mteule Dr. John Pombe Magufuli ameshinda kwa asilimia 58.46 sawa na kura 8, 882, 935. Itakumbukwa kwamba, Dr. Magufuli alikuwa anapeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi.

Jaji Lubuva anasema, Bwana Edward Lowassa ameshinda kwa asilimia 39. 97 sawa na kura 6, 072, 848 za kura zote zilizopigwa. Kwa matokeo haya, Tume ya Taifa ya Ucahguzi imekata mzizi wa fitina kati ya Chama cha Mapinduzi na Muungano wa Vyama vya Upinzani uliokuwa chini ya mwamvuli wa UKAWA. Hata hivyo Bwana Lowassa aliyewahi kuwa Waziri mkuu wa Tanzania amekataa kukubali matokeo kwa madai kwamba, Tume ya Uchaguzi ya Taifa imechakachua matokeo na kwamba, mshindi halali ni Bwana Lowassa.

Chama cha Mapinduzi kinasherehekea ushindi wa Dr. John Pombe Magufuli, wakati ambapo kuna vigogo wa CCM wakiwa wamepigwa mweleka, chali na vyama vya upinzani. Wachunguzi wa mambo wanasema,. Hapana shaka kwamba, watanzania wamechoka na uongozi wa mazoea, sasa ni kazi hadi kieleweke, wavivu watafute mahali pa kwenda! Dr. John Pombe Magufuli, Alhamisi tarehe 29 Oktoba 2015 anasherehekea Siku yake ya kuzaliwa, kwa kutimiza miaka 56.

Wakati huo huo viongozi wa kidini wanapenda kuwahamasisha watanzania wote kuhakikisha kwamba, wanaonesha ukomavu wa kisiasa na kidekomrasia kwa kujikita katika misingi ya haki, amani na utulivu. Wale walioshindwa katika uchaguzi mkuu uliopita waoneshe mshikamano na umoja wa kitaifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote. Kwa wale ambao hawataridhika, basi wafuate sheria, taratibu na kanuni za nchi ili haki iweze kutendeka!

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.